Safari ya Mogherini Tehran, mashauriano kuhusu masuala ya kieneo
Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya leo asubuhi amekutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran kuhusu masuala ya pande mbili, matukio ya kieneo na kimataifa.
Moja ya masuala makuu yaliyojadiliwa na Mogherini katika mazungumzo yake hapa Tehran ni kuhusu matukio ya hivi karibuni ya kieneo na pia hali ya mambo ya Syria. Kustafidi na suhula na uwezo wa kidiplomasia wa kieneo wa Iran kuhusu kuipatia ufumbuzi mizozo ya kieneo ni miongoni mwa masuala muhimu katika mazungumzo ya kisiasa kati ya Iran na nchi za Ulaya. Ni katika mkondo huo ndio maana mazungumzo kati ya Iran na maafisa wa siasa za nje wa Umoja wa Ulaya hapa Tehran yakahesabiwa kuwa ni mazungumzo yenye umuhimu mkubwa.
Iran imeanza kufanya majadiliano muhimu na nchi za Ulaya baada ya kutekelezwa mpango wa JCPOA. Mazungumzo hayo yameingia katika ukurasa mpya kufuatia safari za miezi kadhaa iliyopita za Bi Federica Mogherini Mkuu wa Siasa za Nje wa Umoja wa Ulaya hapa nchini. Azimio la stratejia mpya ya Umoja wa Ulaya kuhusu Iran baada ya makubaliano ya nyuklia ambalo lilipasishwa wiki iliyopita limeyapa kasi mpya mazungumzo hayo. Azimio hilo limekiri kuhusu nafasi chanya iliyonayo Iran kimataifa na katika eneo katika kurejesha amani na uthabiti katika eneo; na kusisitiza pia kushiriki Iran katika kuipatia ufumbuzi mizozo na mivutano ya kieneo na katika mapambano dhidi ya ugaidi, khususan vita dhidi ya Daesh na makundi mengine kama hayo na kusisitiza pia kuimarishwa uhusiano wa pande mbili katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, nishati, sayansi, elimu, utafiti na mazingira.
Kwa mtazamo huo, mazungumzo ya aina hiyo kwa kuzingatia mitazamo ya Umoja wa Ulaya kuhusu masuala ya kisiasa ya eneo, yanaweza kuwa chachu ya kuimarishwa mshikamano wa kisiasa na kusaidia kurejesha amani na uthabiti katika eneo. Licha ya kuwa Iran na nchi za Ulaya hazina mitazamo inayofanana katika masuala yote, lakini pande mbili hizo zina misimamo ya pamoja kuhusu masuala kadhaa muhimu ya kieneo na kimataifa. Umoja huo unaweza kupelekea kufanyika mazungumzo ya maana kwa ajili ya kutatua matatizo mbalimbali na vitisho vya pamoja dhidi yao.
Akizungumza hapa Tehran miezi kadhaa iliyopita na Matteo Renzi Waziri Mkuu wa Italia, Ayatullah Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alikosoa miamala ya kindumakuwili ya Marekani na baadhi ya nchi za Ulaya khususan katika suala la kupambana na ugaidi na kueleza kuwa, nchi hizo ambazo zinajiiita muungano wa mapambano dhidi ya ugaidi zinaeneza propaganda za kuidhihirisha dini ya Uislamu kuwa ni tishio badala ya kuendesha vita vya kweli dhidi ya magaidi. Ni wazi kuwa uhakika huu wa mambo hauwezi kufichika kwa upande wa Iran; na ni uthibitisho kuhusu aina na kiwango cha uhusiano uliopo kati ya Iran na nchi za Ulaya.
Mazungumzo haya yanafanyika katika hali ambayo Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Russia na Syria jana Ijumaa walikuwa na kikao cha pamoja huko Moscow Russia ikiwa ni katika kuendeleza jitihada zao za kufanikisha mapambano dhidi ya ugaidi huko Syria na kuupatia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo kwa njia ya kisiasa.
Muhammad Javad Zarif Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliashiria katika mkutano na waandishi wa habari huko Moscow kwamba, hatari ya ugaidi haiihusu Syria na eneo hili pekee, bali ni tishio kwa ulimwengu mzima na kubainisha kuwa, Russia, Syria na Iran zinaendelea kuzidisha jitihada zao katika vita dhidi ya ugaidi na kulinda misingi ya haki za binadamu. Pande nyingi zinahusika katika kushadidisha mgogoro huko Syria huku kukiwepo pia hitilafu nyingi za kimitazamo katika uga wa kimataifa kuhusu namna ya kuutatua mgogoro wa nchi hiyo. Hadi sasa hakuna njia madhubuti na ya pamoja iliyopatikana ya kuupatia ufumbuzi mgogoro wa Syria. Hata kama hadi sasa makundi ya kigaidi yamepata hasara na kipigo kikali huko Syria, lakini hiyo pekee haitoshi. Hii ni kwa sababu,ili kuweza kuupatia suluhisho mgogoro wa Syria, kwanza uungaji mkono wa kifedha na silaha kwa makundi ya kigaidi unapasa kukomeshwa na pili matakwa ya wnanachi wa Syria yanapaswa kuzingatiwa. Weledi wa mambo wanaamini kuwa, hali ya kisiasa na kijeshi itakuwa tata zaidi huko Syria iwapo mazungumzo ya Wasyria kwa Wasyria hayatazaa matunda.