Hatimaye Lebanon yapata Rais; Michel Aoun achaguliwa kuwa Rais
Hatimaye baada ya miaka miwili na nusu ya kutokuwa na Rais, Lebanon leo imepata Rais mpya wa nchi hiyo baada ya Michel Aoun kuchaguliwa kushika wadhifa huo.
Bunge la Lebanon leo limemchagua Michel Aoun jenerali wa zamani wa jeshi na kiongozi wa mrengo wa mabadiliko kuwa rais wa 13 wa nchi hiyo.
Baada ya Michel Aoun kuibuka na ushindi aliapishwa na hivyo ndiye Rais mpya wa Lebanon. Wananchi wa Lebanon hasa mahala alipozaliwa Michel Aoun walimiminika barabrani kushangilia ushindi huo.
Bunge la Lebanon limemchagua Rais mpya wa nchi hiyo baada ya kushindwa kufanya hivyo kwa muda wa zaidi ya miaka miwili kutokana na kukabiliwa na mkwamo wa kisiasa.
Katika uchaguzi wa leo katika Bunge la Lebanon, Michel Aoun alishindwa kupata theluthi mbili ya kura na hivyo uchaguzi huo kuingia duru ya pili. Hata katika duru ya pili na ya tatu pia mambo yalikuwa magumu pia ambapo uchaguzi huo ulazimika kuingia katika duru ya nne. Katika duru ya nne Michel Aoun alipata kura 83 kati ya 127 za Wabunge na hivyo kuwa Rais wa nchi hiyo.
Tangu tarehe 25 Mei 2014 baada ya kumalizika kipindi cha urais wa Michel Suleiman, Lebanon imekumbwa na ombwe la kisiasa kwa kubaki bila ya kuwa na rais kutokana na bunge kushindwa kufikia mwafaka juu ya mtu atakayejaza nafasi iliyoachwa wazi na Michel Suleiman.