Walowezi wa Kizayuni washambulia tena Masjidul Aqsa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i19201-walowezi_wa_kizayuni_washambulia_tena_masjidul_aqsa
Kwa mara nyingine tena walowezi wa Kizayuni wamekishambulia kibla cha kwanza cha Waislamu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Nov 10, 2016 09:54 UTC
  • Walowezi wa Kizayuni washambulia tena Masjidul Aqsa

Kwa mara nyingine tena walowezi wa Kizayuni wamekishambulia kibla cha kwanza cha Waislamu.

Shirika la habari la Ma'an limeripoti kuwa, walowezi wa Kizayuni wapatao 100 wameushambulia Msikiti wa al-Aqsa, wakiwa chini ya ulinzi na himaya ya askari wa utawala haramu wa Israel.

Wakfu unaosimamia masuala ya msikiti huo umeripoti kuwa, licha ya sheria za kimataifa kuzuia walowezi wa Kiyahudi kuhujumu msikiti huo na matukufu mengine ya kidini, lakini kwa mara nyingine tena Jumatano  ya jana waliushambulia chini ya ulinzi wa vyombo vya usalama vya utawala huo wa Kizayuni.

Msikiti wa al-Aqsa

Jumatatu iliyopita, Yuli Edelstein, Spika wa Bunge la Israel (Knesset) aliungana na mawaziri watatu na wabunge watatu wa utawala huo haramu, kuzindua lobi na kampeni za kuuyahudisha msikiti  wa al-Aqsa, kibla cha kwanza cha Waislamu.

Walowezi wa Kiyahudi wakisaidiwa na askari wa Israel wamekuwa wakifanya jitihada za kuharibu eneo hilo tukufu na mikakati inafanyika usiku na mchana ili kubadili utambulisho na nembo zote za Kiislamu na Kikristo za mji wa Baitul Muqaddas (Jerusalem) na kuweka mahala pale nembo na alama za Kiyahudi.

Masjidul Aqsa ni msikiti wa tatu kwa utukufu kwa Waislamu, baada ya Masjidul Haraam (Kaaba) mjini Makka na Masjidu Nabawi mjini Madina.