Wapalestina wamkosoa Kenyatta kwa kutembelea Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1981-wapalestina_wamkosoa_kenyatta_kwa_kutembelea_israel
Maafisa wa serikali ya Palestina wamemkosoa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwa kutembelea vitongoji haramu huko Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 26, 2016 12:45 UTC
  • Wapalestina wamkosoa Kenyatta kwa kutembelea Israel

Maafisa wa serikali ya Palestina wamemkosoa Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya kwa kutembelea vitongoji haramu huko Israel katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Mapema wiki hii Rais Kenyatta alitembelea ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kukutana na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu mjini al-Quds (Jerusalem). Akiwa huko alikutana pia na wanafunzi Wakenya walioko katika kitongoji cha Wazayuni katika eneo linalokaliwa kwa mabavu la Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO imelaani safari hiyo katika taarifa iliyotolewa Alhamisi. PLO imesema mikataba ya kimataiifa inatambua ardhi za Palesitna zilizokaliwa na Israel mwaka 1967 kuwa sehemu ya taifa la Palestina na hivyo hakuna yeyote aliye na haki ya kutembelea ardhi hizo pasina kushauriana na uongozi wa Palestina.

Afisa mwandamizi wa Palestina Hanan Ashrawi amesema safari hiyo itaupa nguvu utawala ghasibu wa Israeli na kuonyesha kuwa Kenya inashirikiana na utawala huo unaokalia ardhi za Palestina kwa mabavu. Amesema PLO italalamikia safari ya Kenyatta katika taasisi za kieneo ukiwemo Umoja wa Afrika. "Safari hiyo imekiuka majukumu ya Kenya ya kutotambua hali iliyoibuliwa kupitia utumiaji nguvu kinyume cha sheria. Safari hiyo pia imekiuka sheria zingine za kimataifa," amesema Katibu Mkuu wa PLO Saeb Erekat. Rais Kenyatta pia amekosolewa kwa kuwataja Wakenya kuwa watu "wenye ujuzi wa kuiba" katika hotuba aliyoitoa alipowahutubua Wakenya huko Israel. Aidha aliendelea kuwataja Wakenya kuwa ni watu wenye ujuzi wa "kutukanana, kufanya mambo mengine maovu na kuleta ukabila".