PCC: Mamia ya watoto wa Palestina wanashikiliwa katika jela za Israel
Taasisi moja isiyokuwa ya serikali huko Palestina imeripoti kuwa, mamia ya watoto wadogo wa Kipalestina wanashikiliwa katika jela za utawala ghasibu wa Isarel.
Taarifa iliyotolewa na Klabu ya Wafungwa wa Palestina katika Jela za Israel (PPC) imesema kuwa, watoto wadogo zaidi ya 200 wa Kipalestina walitiwa nguvuni mwaka 2015 na kwamba wengi miongoni mwao walikamatwa katika eneo la Quds (Jerusalem).
Taarifa hiyo ambayo imetolewa kabla ya maadhimisho ya Siku ya Watoto Duniani inayosherehekewa tarehe 20 Novemba, imeashiria uhalifu na jinai zinazofanywa na utawala wa Kziayuni wa Isarel dhidi ya watoto wa Palestina kama kuwafyatulia risasi kwa makusudi, kuwatia jela bila ya kuwapa chakula au maji, kuwatesa kwa kuwapiga, matusi na kadhalika.
Taarifa hiyo ya taasisi ya PCC imetolewa sambamba na hatua ya Isarel ya kumhamishia Mpalestina Ahmad Saleh Manasra mwenye umri wa miaka 14 katika jela yenye ulinzi mkali ya Megiddo.
Tarehe 7 Novemba mahakama ya Jerusalem ilimhukumu mtoto huo wa kipalestina kifungo cha miaka 12 jela kwa madai ya kujaribu kumuua mlowezi wa Kiyahudi huko Quds Mashariki inayokaliwa kwa mabavu Octoba 12, 2015.
Zaidi ya Wapelestina 260 wakiwemo watoto wameuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Israel tangu mwanzoni mwa mwezi Octoba mwaka jana.