Askari watano wa Marekani wauawa kaskazini mashariki mwa Syria
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, wanajeshi watano wa Marekani na wanamgambo wawili wa Kikurdi wameuawa katika kambi moja ya kijeshi inayomilikiwa na magenge ya kigaidi katika kiunga cha mji wa Hasakah, kaskazini mashariki mwa Syria.
Televisheni ya TRT ya Uturuki imeripoti habari hiyo na kusema kuwa kambi hiyo ya kijeshi iko katika eneo la Tall-at Tamr, katika kiunga cha mji wa Hasakah nchini Syria.
Nalo kundi la Haki za Binadamu la Syria linaloyaunga mkono magenge ya kigaidi lenye makao yake mjini London, Uingereza, nalo limethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, kumesikika miripuko mitano ya mfululizo katika kambi hiyo ya kijeshi iliyoko chini ya wanajeshi wa Marekani.
Wakati huo huo, Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema watoto karibu nusu milioni katika sehemu mbali mbali nchini Syria wanaishi chini ya mzingiro na hali ngumu ya maisha.
Anthony Lake, Mkurugenzi Mkuu wa UNICEF amesema kati ya watu milioni 4 wanaoishi katika hali ngumu ya maisha nchini Syria, zaidi ya laki 5 ni watoto wadogo. Amesema watoto laki tano katika maeneo 16 ya nchi hiyo wapo chini ya mzingiro kwa zaidi ya miaka miwili, wengi wao wakikosa huduma za msingi na za kibinadamu. Ameongeza kuwa, watoto wapatao laki moja wanapitia kipindi kigumu cha maisha, mashariki mwa mji wa Aleppo pekee, eneo ambalo lingali chini ya udhibiti wa kundi la kigaidi na la wakufurishaji la Daesh (ISIS).
Tangu mwezi Agosti mwaka 2014, Marekani na waitifaki wake wamekuwa wakifanya mashambulizi ya anga nchini Syria kwa kisingizio cha kupambana na magaidi wa Daesh (ISIS) bila ya kibali cha Umoja wa Mataifa na bila ya idhini ya serikali ya Damascus. Hadi hivi sasa muungano huo umeshaua mamia ya raia wa nchi hiyo ya Kiarabu wasio na hatia sambamba na kuharibu makazi yao.