Wanaharakati watatu wa Kishia wahukumiwa kunyongwa Saudia
Mahakama moja ya Saudi Arabia imewahukumu kunyongwa wanaharakati watatu wa Kishia wa nchini humo.
Wanaharakati hao watatu wanatoka katika eneo la Qatif nchini Saudi Arabia ambalo wakazi wake wengi ni Waislamu wa madhehebu ya Shia. Mahakama hiyo ya Saudia imemhukumu pia mwanaharakati mwingine wa Kishia kifungo cha miaka 12 jela. Wanaharakati hao wa Kishia wametuhumiwa kwa kuendesha mapambano ya silaha dhidi ya utawala wa Aal Saud. Maeneo ya Qatiif na Ahsaa huko mashariki mwa Saudi Arabia katika miaka ya hivi karibuni yamekuwa yakishuhudia wimbi kubwa la utiwaji mbaroni wanazuoni, maulamaa, wanaharakati na hata raia wa kawaida unaofanywa na askari usalama wa utawala wa Aal Saud.
Utawala wa Aal Saud unaatekeleza hukumu za kuwatia mbaroni na kuwanyonga raia wa nchi hiyo katika hali ambayo aghalabu ya watuhumiwa hushtakiwa kwa makosa ya uhalifu kutokana na sababu za kisiasa na kuelekezewa tuhuma zisizo na msingi. Utawala wa Aal Saudi unaendeleza ukandamizaji mkubwa dhidi ya wanaharakati wa kisiasa na watetezi wa haki za binadamu nchini humo na pia kuwahukumu kunyongwa kwa kisingizio eti cha kuendesha mapambano dhidi ya ugaidi; huku siasa hizo zikikosolewa pakubwa na jumuiya za kutetea haki za binadamu kama Shirika la Amnesty International, Human Rights Watch na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.