Walowezi wa Kiyahudi wauvunjia heshima tena msikiti wa al-Aqswa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i20761-walowezi_wa_kiyahudi_wauvunjia_heshima_tena_msikiti_wa_al_aqswa
Makumi ya walowezi wa Kiyahudi jana Jumapili waliuvamia Msikiti Mtukufu wa al Aqsa katika mji wa Baitul Muqaddas na kulivunjia heshima eneo hilo tukufu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Dec 05, 2016 00:40 UTC
  • Walowezi wa Kiyahudi wauvunjia heshima tena msikiti wa al-Aqswa

Makumi ya walowezi wa Kiyahudi jana Jumapili waliuvamia Msikiti Mtukufu wa al Aqsa katika mji wa Baitul Muqaddas na kulivunjia heshima eneo hilo tukufu.

Ripoti kutoka Palestina zinasema kuwa, walowezi wa Kiyahudi wasiopungua 60 jana walifanya hujuma na uvamizi katika msikiti wa al-Aqswa wakiwa na lengo la kufanya shughuli ya kidini katika msikiti huo mtakatifu.

Katika siku za hivi karibuni, walowezi wa Kiyahudi wamekithirisha vitendo vya kuvamia na kufanya hujuma dhidi ya msikiti wa al-Aqswa vitendo ambavyo vimekuwa vikipata himaya na uungaji mkono wa moja kwa moja wa jeshi la utawala haramu wa Israel. 

Askari wa Israel wakivamia msikiti wa al-Aqswa

Mwezi Oktoba mwaka huu walowezi wa Kiyahudi elfu tatu waliuvamia msikiti wa al-Aqswa na kufanya vitendo vya kulivunjia heshima eneo hilo takatifu. Utawala wa Kizayuni wa Israel umekuwa ukifanya njama za kubadilisha utambulisho wa Kiislamu na Kikristo katika eneo hilo na kuweka nembo na utambulisho wa Kiyahudi. Hata hivyo hatua ya Wapalestina ya kusimama kidete hadi sasa imekwamisha njama za utawala huo ghasibu pamoja na walowezi wa Kiyahudi.

Inafaa kukumbusha hapa kuwa, ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel zinashuhudia wimbi jipya la Intifadha dhidi ya utawala wa Kizayuni kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Hadi hivi sasa Wapalestina karibu mia tatu wameshauawa shahidi na Wazayuni katika Intifadha hiyo iliyopewa jina la Intifadha ya Quds.