Silaha za kisasa za Marekani mikononi mwa magenge ya kigaidi
Habari kutoka nchini Marekani zinasema kuwa, bunge la nchi hiyo limeipa idhini Serikali kuyaimarisha kwa silaha za kisasa magenge ya kigaidi yanayofanya mauaji nchini Syria.
Bunge la Marekani limeipa idhini serikali ijayo ya nchi hiyo kuyapa magenge ya kigaidi na kitakfiri ya nchini Syria, makombora ya kisasa ya kutungulia ndege. Wakati wa kampeni za uchaguzi, rais mteule wa Marekani, Donald Trump alisema kuwa hana mpango wa kuingilia vita vya ndani nchini Syria. Lakini kinyume na ahadi zake za wakati wa kampeni za uchaguzi, amechagua washauri wenye misimamo mikali na wajumbe wa Baraza la Mawaziri ambao ni wapenda vita. Miongoni mwa wajumbe hao ni Jenerali James Mattis ambaye amempendekeza awe Waziri wa Ulinzi wa Marekani. Jenerali Mattis ni maarufu sana kwa misimamo yake ya chuki dhidi ya Waislamu na hususan dhidi ya serikali ya Syria. Mwezi Januani 2015, Jenerali Mattis ambaye ni maarufu kwa jina la "mbwa kichaa," aliliambia Baraza la Sanate kwamba wakati umefika kwa Marekani kuwaunga mkono waasi wa Syria ambao alidai eti wana misimamo ya wastani.
Misimamo ya Marekani kuhusiana na matukio ya hivi sasa ya Syria yanaonesha kuwa, nchi hiyo ina nia ya kuidhoofisha serikali ya Rais Bashar al Assad na kuyatia nguvu magenge ya kigaidi. Marekani inatumia njama za kusimamisha vita na kutofautisha baina ya magaidi wazuri na wabaya huko Syria ili ipate fursa ya kufanikisha siasa zake za kibeberu katika nchi hiyo ya Kiarabu. Katika siku za hivi karibuni, jeshi la Syria limepata mafanikio makubwa katika vita dhidi ya magaidi na limefanikiwa kuwasafisha magaidi hao katika maeneo tofauti ya nchi hiyo. Mafanikio hayo ya jeshi la Syria, yamewatia wasiwasi waungaji mkono wa magaidi hao hasa Marekani. Hivyo Washington imeamua kuwaongezea nguvu magaidi kwa madai ya kutuma misaada ya kibinadamu katika maeneo ambayo magenge ya kigaidi yamezidiwa nguvu na jeshi la Syria.
Huko nyuma pia, Marekani ilitumia mbinu hiyo hiyo ya misaada ya kibidanamu kuwatumia zana za kisasa magaidi nchini Syria. Marekani imekuwa ikizusha mara kwa mara masuala kama usimamishaji vita, kutengwa maeneo salama, kutengwa maeneo yaliyo marufuku kupaa ndege n.k, shabaha yake kuu ikiwa ni kuwafungulia uwanda wa usalama magaidi. Marekani na waungaji mkono wengine wa magenge ya kigaidi wameshindwa hadi hivi sasa kufikia malengo yao hayo. Hivyo wameamua kuwasaidia kwa kila hali magaidi, suala ambalo lina madhara makubwa kwa wananchi na raia wa kawaida wa Syria. Fauka ya hayo, lengo la Marekani ni kuzitia hofu nyoyo za wananchi wa Syria pamoja na walimwengu na kujaribu kuonesha kuwa hali nchini Syria ni mbaya sana. Hata hivyo, njama hizo hazioneshi jambo jingine ghairi ya chuki na hamaki za kibeberu za Marekani kutokana na mafanikio makubwa linayoendelea kupata jeshi la Syria katika vita vyake dhidi ya magaidi.
Hivi sasa Marekani imetilia nguvu uwezekano wa dola hilo la kibeberu kuingilia kijeshi mgogoro wa Syria katika hali ambayo, mauaji dhidi ya raia na uharibifu mkubwa wa miundombinu ya Syria ndiyo matunda ya uvamizi uliofanyika nchini Syria na mauaji ya kigaidi yanayondelea nchini humo kwa miaka sita sasa. Mgogoro wa Syria kwa hakika unachochewa na uingiliaji wa maadui wa taifa hilo lililosimama kidete kupambana na utawala wa Kizayuni wa Israel. Marekani ina nafasi ya moja kwa moja katika matatizo yote hayo.