Assad: Kuikomboa Aleppo, hatua kubwa ya kumaliza vita Syria
Rais Bashar al-Assad wa Syria amesema iwapo jeshi la nchi hiyo litafanikiwa kuukomboa mji wa Aleppo, itakua ni hatua kubwa ya kuelekea kumaliza vita na harakati za kigaidi katika nchi hiyo.
Kanali ya televisheni ya al-Mayadeen imenukuu kauli hiyo ya Assad aliyoisema katika mahojiano na gazeti la al-Watan na kuongeza kuwa, kuukomboa mji wa Aleppo ulioko kaskazini magharibi mwa nchi itakuwa pigo kwa magenge ya kigaidi na waungaji mkono wao kieneo na kimataifa.
Rais wa Syria amesema kuwa, Marekani inashinikiza usitishaji vita wa muda Aleppo, kutokana na pigo na hali ngumu wanayoipitia mamluki wake wa kigaidi katika mji huo. Amesisitiza kuwa, iwapo magenge ya kigaidi yatasambaratishwa na kutokomezwa katika mji huo, basi mkondo wa vita nchini Syria utabadilikia kikamilifu na kupata sura mpya, kuelekea ushindi.
Jeshi la Syria limeendelea kupata mafanikio na kusonga mbele katika maeneo mengi yaliyokuwa yakidhibitiwa na makundi ya magaidi hususan Daesh/ISIS.
Mapema wiki hii, jeshi hilo lilitangaza kuwa, wanachama 50 wa kundi la kigaidi la Jaish al-Fat'h wameuawa katika operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya ngome za magaidi hao katika viunga vya miji ya Idlib na Hama.
Makundi ya kigaidi na wapinzani wa serikali ya Rais Assad wamekiri kuwa, wapiganaji wao wamepoteza kikamilifu udhibiti wa eneo la kaskazini mashariki mwa Aleppo ambalo kwa sasa lipo chini ya udhibiti wa jeshi la nchi hiyo. Imearifiwa kuwa, jeshi la Syria linadhibiti zaidi ya asilimia 60 ya mji huo wa kistratajia.