Kubomolewa zaidi ya nyumba 800 za Wapalestina na askari wa Israel
(last modified Fri, 16 Dec 2016 02:39:32 GMT )
Dec 16, 2016 02:39 UTC
  • Kubomolewa zaidi ya nyumba 800 za Wapalestina na askari wa Israel

Wakuu wa jumbe za Umoja wa Ulaya walioko Batul Muqaddas na Ramallah huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu wameripoti kuwa tangu ulipoanza mwaka huu wa 2016 hadi sasa askari wa utawala wa Kizayuni wa Israel wamebomoa zaidi ya nyumba 800 za Wapalestina.

Wakuu hao wa jumbe za Umoja wa Ulaya wametaka kukomeshwa mwenendo huo wa bomoabomoa ya nyumba za Wapalestina. Tangu ulipoanza mwaka huu, utawala wa Kizayuni umezidisha kasi ya unyang'anyi wa ardhi za Wapalestina kwa ajili ya kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni. Kwa mujibu wa ripoti, tangu ulipoanza mwaka huu hadi sasa, uporaji na unyang'anyi wa ardhi za Wapalestina umeongezeka kwa kiwango cha asilimia 439 kulinganisha na mwaka uliopita. Kubomoa nyumba na kupora ardhi za Wapalestina kwa kutumia njia tofauti ikiwemo ya utungaji sharia za kionevu, kuweka mpaka wa utoaji vibali vya ujenzi kwa Wapalestina, kuzipora ardhi zao, kuyatumia makundi ya kidini na ya kufurutu mpaka katika ujenzi wa vitongoji na vilevile kueneza hofu na vitisho kwa Wapalestina, yote hayo yanafanyika kwa lengo la kuhakikisha hakuna Mpalestina anayesalia katika mji mtukufu wa Quds.

Taswira ya mji wa Baitul Muqaddas

Kuwabomolea Wapalestina nyumba zao na kupanua ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni ni mojawapo ya siasa na sera hatari zaidi zinazotekelezwa na utawala haramu wa Kizayuni wa Israel. Mpango huo unakinzana na maslahi ya Wapalestina. Kubadilisha muundo wa kijiografia wa maeneo ya Wapalestina na kuyapa sura ya Kiyahudi na Kizayuni ni miongoni mwa malengo yanayofatiliwa na utawala ghasibu wa Israel. Kulitenganisha kikamilifu eneo la mashariki na mji mzima wa Baitul Muqaddas ni mojawapo ya sababu ya kupingwa mpango huo kimataifa.

Kutekelezwa mpango huo kutaondoa uwezekano wa Wapalestina kujistawisha kuelekea upande wa mashariki. Kwa upande mwingine, mpango huo utazuia kuwepo eneo la Baitul Muqaddas Mashariki lililokusudiwa kuwa mji mkuu wa nchi ya Palestina. Kwa utaratibu huo Baitul Muqaddas iliyokusudiwa kuwa mji mkuu wa serikali ya Palestina haitokuwa na nafasi yoyote ya kupumua na kwa kutenganishwa na maeneo mengine ya Ufukwe wa Magharibi. Utekelezaji mpango huo wa Kizayuni utasababisha madhara kwa maeneo mengi ya ardhi za Palestina. Kwa kutekelezwa mpango huo, maeneo na vijiji vyote vyenye wakaazi Waarabu vitakuwa vimezingirwa na vitongoji vya walowezi wa Kizayuni.

Vitongoji vya walowezi wa Kizayuni

Ujenzi wa vitongoji unaofanywa na Wazayuni utatenganisha maeneo ya upande mmoja ya Wapalestina na upande mwingine na kuwasababishia matatizo mengi mno. Hatari iliyopo ni kwamba hatua ya karibuni ya ubomoaji nyumba za Wapalestina inaweza kuharakisha mpango wa kuanzisha Quds kubwa kulingana na mtazamo wa Israel na kusababisha mabadiliko makubwa na ya msingi katika ramani ya hali ya watu katika Palestina kwa manufaa ya utawala wa Kizayuni. Kwa hakika mpango huo ni ujengaji ukuta mwingine mpya wa Kizayuni. Ukweli ni kwamba serikali moja baada ya nyingine za utawala haramu wa Kizayuni wa Israel zimekuwa zikitekeleza sera ya ujenzi wa vitongoji huku zikijaribu kuviunganisha pamoja vitongoji hivyo kwa madhumuni ya kuutenga mji wa Baitul Muqaddas kutokea mashariki, kaskazini na kusini. Bila kujali lawama zinazotolewa kimataifa dhidi yake, utawala wa Kizayuni unaendeleza na kupanua ujenzi wa vitongoji ili kuimarisha sera na mkakati wake wa kibeberu na wa kujitanua zaidi katika ardhi za Palestina unayoikalia kwa mabavu…/    

 

Tags