Askari na mamluki wa Saudia wazidi kuangamizwa na vikosi vya Yemen
Mamluki wasiopungua 16 wa Saudi Arabia huko nchini Yemen wameangamizwa kufuatia operesheni ya kijeshi ya jeshi la Yemen likisaidiwa na vikosi vya kujitolea vya wananchi.
Kanali ya televisheni ya al-Masira ya Yemen imeripoti kuwa, askari watatu wa Saudia wameuawa kwa kufyatuliwa risasi na vikosi vya Yemen katika eneo la al-Mazraq mkoa wa Jizan na eneo la milima la Tabat al-Hamrah, kusini mashariki mwa Saudia, huku mamluki zaidi ya 10 wa utawala huo wa kifalme wakiuawa katika maeneo mengine ya Yemen.
Aidha mamluki wengine watatu wa Saudia wameuawa katika shambulizi la roketi la vikosi vya Yemen, katika wilaya ya al-Ghayl, kaskazini mwa mkoa wa Jawf.
Haya yanajiri siku tatu baada ya mamluki wasiopungua 97 wa Saudi Arabia huko nchini Yemen kuangamizwa kufuatia operesheni ya kijeshi ya kamati za wananchi huku wengine 50 wakijeruhiwa.
Majeshi ya Saudi Arabia na washirika wake kama Marekani, Israel na nchi kadhaa za Kiarabu, yalianza kulishambulia taifa la Yemen mwezi Machi mwaka jana kwa kisingizio cha kumrejesha madarakani rais aliyetoroka nchi na kukimbilia Saudia, Abd Rabbuh Mansur Hadi.
Mashambulio hayo ya kinyama ya Saudia hadi sasa yameshaua zaidi ya Wayemeni elfu kumi, kujeruhi mamia ya maelfu ya wengine au kuwaacha bila makazi mbali na kuteketeza asilimia 80 ya taasisi za miundombinu na za utoaji huduma na tiba za nchi hiyo masikini ya Kiarabu.