Mapambano, njia pekee ya kuikomboa Palestina
Mkuu wa Tume ya Usalama wa Taifa na Sera za Kigeni katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran amesema mazungumzo baina ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel hayatazaa matunda na kwamba njia pekee ya kuikomboa Palestina ni kupitia mapambano au muqawama.
Allaudin Burujerdi ameashiria mkutano tarajiwa mjini Moscow baina ya Mahmoud Abbas Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel na kusema: "Mamlaka ya Ndani ya Palestina imekuwa ikipata hasara kila mara inapochukua hatua ya mazungumzo ya maelewano na utawala wa Kizayuni."
Burujerdi amesisitiza kuwa, wanamapinduzi wote wa Palestina wamefikia natija kuwa, njia pekee ya ukombozi ni kuendeleza mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel hadi pale ardhi zote za Palestina zitakapokombolewa kikamilifu.
Burujerdi amesisitiza kuwa, Wapalestina wanapaswa kusimamia masuala yao ya ndani pasina uingiliaji wa kigeni.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia Maria Zakharova ametangaza kuwa, Mahmoud Abbas ametangaa kuwa tayari kukutana na Netanyahu mjini Moscow.