Milipuko yaua kwa uchache watu 28 katikati mwa Baghdad, Iraq
(last modified Sat, 31 Dec 2016 14:53:51 GMT )
Dec 31, 2016 14:53 UTC
  • Milipuko yaua kwa uchache watu 28 katikati mwa Baghdad, Iraq

Milipuko miwili iliyotokea katikati mwa mji mkuu wa Iraq, Baghdad imeua watu wasiopungua 28.

Duru za polisi za hospitali zimetangaza kuwa, milipuko hiyo imetokea leo katika eneo la kibiashara la al-Sinek mjini Baghdad.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, mlipuko wa kwanza ulikuwa ni wa bomu la kutegwa garini huku mlipuko wa pili ukitokea baada ya timu ya watoaji misaada kuwasili katika eneo hilo kwa ajili ya kuwasaidia wahanga wa mlipuko huo. 

Watu 54 wanaripotiwa kujeruhiwa katika milipuko hiyo na kwamba, kuna uwezekano wa idadi ya vifo kuongezeka kutokana na hali ya baadhi ya majeruhi wa shambulio hilo la kigaidi kuwa mbaya.

Mlipuko wa leo Baghdad Iraq

Kundi la kigaidi la Daesh limetangaza kuwa, ndilo lililohusika na shambulio hilo. Mlipuko mwingine wa bomu ulitokea siku ya Alkhamisi kusini mwa mji mkuu wa Iraq Baghdad ambapo mtu mmoja aliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa baada ya bomu lililokuwa limetegwa garini kulipuka.

Maafisa wa serikali ya Iraq wametangaza kuwa, makundi ya kigaidi yamebadilisha mbinu na sasa yanawalenga zaidi raia baada ya kushindwa katika medani ya vita hususan katika mkoa wa kaskazini mwa nchi hiyo wa Nainawa.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, viongozi wa Iraq wameendelea kusisitiza azma ya serikali ya nchi hiyo ya kupambana na makundi ya kigaidi kwa hali na mali hadi itakapong'oa mizizi ya magaidi yao katika ardhi ya nchi hiyo.