Kuzidi kuwa "ngangari" Wapalestina mbele ya jinai za Israel
(last modified Fri, 13 Jan 2017 02:31:31 GMT )
Jan 13, 2017 02:31 UTC
  • Kuzidi kuwa

Wakazi Waarabu katika mji wa Qalansuwa wa kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina la Israel wameanzisha mgomo wa wote kwa ajili ya kulalamikia hatua ya utawala wa Kizayuni ya kuvunja nyumba zao 11.

Mgomo huo umepelekea kufungwa mashule yote, maduka na taasisi za huduma za watu za maeneo yenye Waarabu wengi ya ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu na Israel. Hayo yamekuja ili kulalamikia hatua ya viongozi wa Israel ya kuvunja nyumba 11 za wakazi Waarabu wa mji wa Qalansuwa. 

Chama cha Orodha ya Pamoja kinachoundwa na vyama vinne vya Waarabu katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni kimetangaza kuwa, serikali ya Benjamin Netanyahu imeamua kuzivunja nyumba hizo ili kuwapotosha watu na kuwafanya wasifuatilie uchunguzi unaofanywa na polisi wa Israel kuhusu ubadhirifu na ufisadi wa kifedha aliofanya Waziri Mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni.

Historia ya utawala wa Kizayuni wa Israel inaonesha kuwa utawala huo pandikizi hausiti kutenda jinai yoyote ile dhidi ya Wapalestina kwa kutumia visingizio tofauti na kwamba Wapalestina hawana amani katika sehemu zote za Palestina.

Jinai kuwavunjia Wapalestina nyumba zao ni jambo la kawaida tangu Wazayuni walipozivamia ardhi za Palestina.

 

Katika miongo ya hivi karibuni, utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha kampeni ya kuwafukuza Wapalestina zaidi ya milioni moja kutoka katika ardhi zao zinazokaliwa kwa mabavu tangu mwaka 1948 na hatimae kuitangaza Israel kuwa ni dola la Mayahudi. Sasa jambo hilo linatumiwa kama kisingizio na utawala wa Kizayuni wa Israel katika kuvunja nyumba za Wapalestina na kuwaondoa kwa nguvu Wapalestina kwenye maeneo yao.

Hivi sasa hatua za ukandamizaji na za kibaguzi zinazochukuliwa na Israel zimechukua mkondo wa hatari zaidi. Wapalestina wanaoishi katika maeneo yaliyotekwa na Wazayuni mwaka 1948 wanakumbwa na ubaguzi wa kila namna na kunafanyika propaganda kubwa za kuwapokonya utambulisho wao kwa kudaiwa eti ni Waarabu wa Israel. Kimsingi Waarabu hao hawapewi haki yoyote kwa kiwango wanachopewa Wazayuni na wanaishi katika mazingira magumu sana. Ubaguzi na unyanyasaji huo unaonekana wazi katika masuala ya elimu, huduma za lazima pamoja na masuala ya kiuchumi na kijamii.

Licha ya utawala wa Kizayuni kutumia hila tofauti kama vile kuwalazimisha Waarabu hao kuchukua uraia wa Israel, lakini umeshindwa kuwapokonya wakazi hao utambulisho wao wa Kipalestina kama ambavyo pia umeshindwa kuwaingiza kwenye jamii ya Israel.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni, anafuatiliwa na polisi kwa ufisadi mkubwa wa fedha

 

Kushtadi ukandamizaji wa utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina kunazidi kubainisha kuwa, viongozi hao wa utawala vamizi wa Quds, hadi hivi sasa wameshindwa kuwa na welewa sahihi kuhusu taifa la wanamuqawama la Palestina, licha ya kupita miaka mingi ya kuishi nao. Katika kipindi chote hiki cha miaka ya muqawama na mapambano yao, wananchi wa Palestina wamethibitisha kuwa kamwe hawawezi kuachana na malengo yao matukufu. Maandamano makubwa ya kupinga utawala wa Kizayuni yanayoshuhudiwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Israel tangu mwaka 1948 ni ushahidi wa wazi wa kuonesha namna Wazayuni walivyoshindwa kuwavua Wapalestina utambulisho wao wa asili licha ya kupita makumi ya miaka tangu walipoziteka na kuzikalia kwa mabavu ardhi zao. Amma kiti kinachotarajiwa hivi sasa na Wapalestina yaani katika wakati huu ambapo vitendo vya kibaguzi vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina vimechukua mwelekeo wa hatari zaidi, ni jamii za kimataifa kuchukua hatua kali za kukabiliana na vitendo vilivyo dhidi ya ubinadamu vinavyofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel ambao lengo lake kuu ni kukifuta kabisa kizazi cha Wapalestina kwenye ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Tags