Umoja wa Mataifa walaani hatua ya Bahrain kuwanyonga wanaharakati
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i23533-umoja_wa_mataifa_walaani_hatua_ya_bahrain_kuwanyonga_wanaharakati
Umoja wa Mataifa umelaani vikali hatua ya utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain ya kuwanyonga wanaharakati watatu kwa madai bandia ya kuhusika na shambulizi la kigaidi la mwaka 2014.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jan 15, 2017 10:57 UTC
  • Umoja wa Mataifa walaani hatua ya Bahrain kuwanyonga wanaharakati

Umoja wa Mataifa umelaani vikali hatua ya utawala wa Aal-Khalifa wa Bahrain ya kuwanyonga wanaharakati watatu kwa madai bandia ya kuhusika na shambulizi la kigaidi la mwaka 2014.

Agnes Callamard, Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya mauaji ya kiholela na udikteta amesema kuwa, wanaharakati hao wameuawa pasina kuwepo ushahidi juu ya madai wanayolimbikiziwa.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa, utawala wa Manama umewanyonga wanaharakati Abbas al-Samea, Ali al-Singace na Sami Mushaima baada ya kuteswa, kudhalilishwa na kuhukumiwa pasina ushahidi madhubuti. Agnes Callamard ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kuwa: "Hakukuwepo haki na uadilifu katika mchakato wa kusikilizwa kesi dhidi ya wanahakarati hao, haya ni mauaji ya kiholela yanayopasa kulaaniwa kwa nguvu zote."

Vijana wanaharakati walionyongwa na utawala wa Bahrain

Kabla ya kutekelezwa hukumu hiyo hii leo, wananchi wa Bahrain tangu jana Jumamosi katika mji mkuu Manama na maeneo ya Diraz, Bani Jamra na Sanabis wamefanya maandamano makubwa kulalamikia hatua ya mahakama ya rufaa ya nchi hiyo ya kupasisha hukumu ya kunyongwa vijana hao.

Itakumbukwa kuwa, Tarehe 9 mwezi huu wa Januari, mahakama ya rufaa ya Bahrain ilipasisha hukumu ya kunyongwa vijana hao watatu kwa madai ya kuhusika na mauaji ya maafisa wa polisi na kutega bomu, licha ya vijana hao kukanusha vikali madai hayo.

Vyombo vya usalama vya utawala wa Aal-Khalifa vimekuwa vikitumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya amani ya wananchi ambao wanapinga serikali ya Manama, tangu mwanzoni mwa mwaka 2011.