UN yatahadharisha kuhusu mgogoro wa kibinadamu Yemen
Mkurugenzi wa Oparesheni za Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusu mgogoro na hatari ya njaa huko Yemen.
Stephen O'Brien amesema katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuwa, mzozo wa Yemen umekuwa suala la dharura kwa ajili ya usalama wa chakula duniani na kwamba njaa inahatarisha maisha ya mamia ya maelfu ya raia wa Yemen iwapo hatua za haraka hazitachukuliwa.
O'Brien ameongeza kuwa, watoto wa Yemen wanasumbuliwa na hali mbaya zaidi kwa sababu watoto wapatao milioni mbili na laki mbili wanakabiliwa na lishe duni huku makumi ya watoto walio na umri wa chini ya miaka kumi wakiaga dunia kila siku.
Maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema kuwa, uvamizi na mashambulizi ya jeshi la Saudi Arabia na waitifaki wake yaliyoanza yapata miaka miwili na nusu iliyopita yameua zaidi ya raia elfu kumi wa Yemen wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo.