Hamas yaionya Israel isijaribu kuishambulia Ghaza
(last modified Thu, 16 Feb 2017 04:06:55 GMT )
Feb 16, 2017 04:06 UTC
  • Hamas yaionya Israel isijaribu kuishambulia Ghaza

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS ameuonya utawala wa Kizayuni wa Israel usijaribu kuichokoza na kuanzisha vita dhidi ya Ukanda wa Ghaza.

Khalid Mashál alisema hayo jana (Jumatano) katika kikao cha "Kadhia ya Palestina: Tathmini ya Mkakati wa 2016 na Makisio ya Stratijia ya 2017" kilichofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Crown Plaza mjini Beirut Lebanon kwamba utawala wa Kizayuni unaitishia HAMAS kuwa utaanzisha vita vingine na HAMAS nayo inauonya utawala huo kwamba harakati hiyo haina chaguo jengine isipokuwa muqawama na kujihami kwa nguvu zake zote. Mashál ameshiriki kwenye kikao hicho kwa njia ya video.

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS ameongeza kuwa, taifa la Palestina linatumia mbinu za kisasa za kupambana na utawala wa Kizayuni na katika mazingira yoyote yale, na kamwe hawawezi kurejea makosa ya watu wengine.

Khalid Mashál, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya HAMAS

 

Aidha ametaka kuboreshwa hali ya ndani ya Palestina ikiwa ni pamoja na kumalizwa hitilafu za mirengo ya ndani ya Palestina na kuzipulizia roho mpya taasisi za kitaifa za Palestina.

Mkuu huyo wa ofisi ya kisiasa ya HAMAS ametilia mkazo udharura wa kufikiwa makubaliano baina ya Wapalestina wote kuhusu mkakati wa pamoja wa kitaifa kwa ajili ya kujihami mbele ya njama na jinai za Israel sambamba na kupewa makundi ya muqawama na ya kitaifa ya Palestina suhula zote za kuweza kupambana vilivyo na Wazayuni.

Baada ya kumalizika vita vya Ghaza mwaka 2014, utawala wa Kizayuni umekuwa ukikiri mara kwa mara uwezo na nguvu za makundi ya muqawama ya Palestina katika kujihami na kukabiliana na Israel.

Tags