Kupanuka wigo wa kuchukiwa kimataifa utawala wa Kizayuni wa Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i25550-kupanuka_wigo_wa_kuchukiwa_kimataifa_utawala_wa_kizayuni_wa_israel
Hatua ya serikali ya Indonesia ya kukataa ndege iliyokuwa imembeba Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel kupita katika anga yake imethibitisha kwamba, kinyume na fikra potofu za Wazayuni, nchi za Kiislamu zingali zinaunga mkono haki za wananchi wa Palestina mbele ya watenda jinai na utawala huo umetengwa kikamilifu kimataifa.
(last modified 2025-10-31T09:05:42+00:00 )
Feb 24, 2017 02:34 UTC
  • Kupanuka wigo wa kuchukiwa kimataifa utawala wa Kizayuni wa Israel

Hatua ya serikali ya Indonesia ya kukataa ndege iliyokuwa imembeba Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel kupita katika anga yake imethibitisha kwamba, kinyume na fikra potofu za Wazayuni, nchi za Kiislamu zingali zinaunga mkono haki za wananchi wa Palestina mbele ya watenda jinai na utawala huo umetengwa kikamilifu kimataifa.

Benjamin Netanyahu akiwa na lengo la kuonyesha kwamba, utawala ghasibu wa Israel haujatengwa kimataifa, awali alifanya safari kusini mwa Asia kwa kuitembelea nchi ya Singapore na akiwa na lengo la kuelekea Australia ndege yake iliomba kupita katika anga ya Indonesia, ombi ambalo lilipingwa na serikali ya Jakarta. Netanyahu ambaye mwaka uliopita ombi lake la kutaka kuweko uhusiano baina ya Israel na serikali ya Indonesia lilikataliwa, hatua yake ya kuomba kupita katika anga ya nchi hiyo ilikuwa na lengo la kuitia katika hali ngumu Jakarta katika kuchukua maamuzi, lakini serikali ya Indonesia ikatumia busara na hekima na kupinga takwa hilo la Wazayuni.

Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel

Hatua hiyo ya Indonesia unahesabiwa kuwa ni dhoruba kali kwa Benjamin Netanyahu hasa kwa kuzingatia kuendelea Intifadha mpya ya wananchi wa Palestina inayojulikana kama Intifadha ya Quds ambayo imeteteresha uhai wa kisiasa wa Wazayuni. Indonesia ambayo ni nchi ya Kiislamu yenye idadi kubwa zaidi ya Waislamu duniani imeendelea kuwa mpinzani wa utawala wa Kizayuni wa Israel na wakati huo huo imekuwa ikiunga mkono haki za wananchi wa Palestina.

Hata kama baadhi ya watawala wa nchi za Kiarabu wameyapa kisogo matukufu ya wananchi wa Palestina na sasa wanachezea katika ulingo wa Wazayuni, lakini Waislamu wenye fikra huru duniani wameonyesha kwamba,  hawako tayari kwa namna yoyote ile kuukubali uwepo wa Wazayuni. Sambamba na hatua ya Indonesia ya kukataa ndege iliyombeba Netanyahu kupita katika anga yake, Muhammad  Saleh Spika wa Baraza la Wawakilishi la Indonesia ambaye alishiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Kuunga Mkono Palestina uliomalizika siku ya Jumatano hapa mjini Tehran alitangaza kuwa, pamoja na kuwa, kuna umbali wa maelfu ya kilomita kati ya Indonesia na Palestina lakini daima Jakarta imekuwa ikitangaza mshikamano wake na wananchi wa Palestina.

Aidha alisisitiza kuwa, wananchi wa Palestina hawako peke yao katika mapambano yao ya Intifadha kwani Indonesia ingali inaendelea kuwaunga mkono kikamilifu.

Kwa kuzingatia nafasi muhimu iliyonayo Indonesia katika Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM, utawala haramu wa Israel unafanya juhudi za kuwa na uhusiano na Jakarta ili uidhoofishe jumuiya hiyo kuhusiana na kadhia ya Palestina; ingawa hadi sasa haujafanikiwa katika hilo. Safari ya Amin bin Haji Mulia spika wa Bunge la Malaysia ambayo ni nchi ya pili muhimu ya Kiislamu ya eneo la kusini mashariki mwa Asia hapa mjiniTehran na kushiriki katika mkutano wa sita wa kimataifa wa kuunga mkono Intifadha ya Palestina ni jambo linaloonyesha kuwa, njama za Wazayuni za kutaka kuleta mpasuko na mgawanyiko baina ya nchi za Kiislamu kuhusiana na kadhia ya Palestina si tu kwamba, zimegonga mwamba, bali nchi za Kiislamu zinautambua utawala wa Kizayuni wa Israel kwamba, ni chimbuko la ugaidi wa kiserikali na sababu ya ukosefu wa usalama na amani duniani.

Mapambano ya Intifadha ya Palestina

Kwa kuzingatia ukweli huu na wakati huo huo kuendelea kila uchao jinai za Wazayuni dhidi ya wananchi wa Palestina, fikra za walio wengi ulimwenguni nazo zinawapinga vikali Wazayuni. Upinzani mkubwa nchini Australia uliokwenda sambamba na safari ya Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa Israel katika mji wa Sidney ni jambo linalopaswa kuzingatiwa katika uwanja huo.

Aidha hatua ya wanachuo wa Chuo cha Trinity  huko Dublin Ireland ya kupinga hotuba ya balozi wa Israel nchini humo ambayo ilipelekea kufutwa hotuba hiyo ni jambo linaloonyesha dhahir shahir kwamba, upinzani dhidi ya Wazayuni hauishii kwa Waislamu tu, bali hata wanafikra huru na watu ambao wana udiriki wa kweli wa ugaidi wa kiserikali wa Israel wanawapinga Wazayuni popote pale walipo.

Mwenendo huu unazidi kuimarisha Intifadha na mapambano ya Wapalestina siku baada ya siku na wakati huo huo, kuendelea kutengwa Israel  limekuwa ni jinamizi linalouandama utawala huo ghasibu popote uendapo.