HRW: Saudia imetenda jinai za kivita Yemen
Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch limesema kuwa mashambulizi ya anga ya Saudi Arabia yaliyoua raia nchini Yemen ni jinai ya kivita.
Shirika la habari la wanafunzi wa vyuo vikuu wa Iran (ISNA) limemnukuu Ahmad bin Shamsi, mkurugenzi wa kitengo cha Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika cha Human Rights Watch akisema hayo jana na kuongeza kukwa, Yemen hivi sasa imekaribia kutumbukia kwenye janga kubwa la kibinadamu.
Amesema, zaidi ya raia milioni tatu wa Yemen wamekuwa wakimbizi na karibu asilimia 80 ya wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu wanahitajia misaada ya dharura ya kibinadamu.
Ahmad bin Shamsi ametoa ushahidi kutoka katika takwimu zilizotolewa na Mpango wa Chakula Duniani WFP na kusema kuwa, hivi sasa kiwango cha lishe duni ni kikubwa mno hususan kwa watoto wa Yemen kiasi kwamba kati ya kila watu watano, mmoja kati yao anasumbuliwa na tatizo hilo.
Mkurugenzi wa Shirika la Haki za Binadamu la Human Rights Watch kitengo cha Mashariki ya Kati na Kaskazini mwa Afrika amegusia pia namna hali ya kibinadamu inavyozidi kuwa mbaya siku hadi siku nchini Yemen na kutaka kuchukuliwe hatua za haraka za kuwaokoa mamilioni ya watu huko Yemen.
Duru za Yemen zinasema kuwa, mashambulizi ya Saudia nchini humo yameshapelekea zaidi ya watu 11 elfu kuuawa na karibu 20 elfu wengine kujeruhiwa. Lengo la Saudia la kuivamia kikatili nchi maskini ya Yemen ni kumrejesha madarakani Abdu Rabuh Mansour Hadi, rais wa zamani wa Yemen aliyejiuzulu na kukimbilia Saudi Arabia.