Mar 16, 2017 04:06 UTC
  • Kazakhstan: Pande zilizoshiriki mazungumzo ya Syria, zimekubaliana kudumisha usitishaji vita

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kazakhstan amesema kuwa, pande zilizoshiriki mazungumzo ya amani ya mjini Astana, mji mkuu wa nchi hiyo, zimekubaliana kudumisha usitishaji mapigano nchini Syria sambamba na kubadilishana mateka.

Kairat Abdurakhmanov ameyasema hayo mwishoni mwa mkutano wa Astana Tatu kuhusiana na mgogoro wa Syria na kuongeza kuwa, mkutano huo ambao ni sehemu ya mkutano ujao wa Geneva, Uswis, umeonyesha matumaini ya uwezekano wa kutatuliwa mgogoro wa nchi hiyo ya Kiarabu.

Kikao cha mazungumzo hayo mjini Astana

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kazakhstan amebainisha kwamba, pande zilizoshiriki mazungumzo ya Astana Tatu, zimekubali kuendeleza usitishaji vita, kubadilishana mateka na watu waliotiwa mbaroni na pande mbili na kadhalika kuunda tume itakayokuwa na jukumu la kusimamia usitishaji vita huo nchini Syria. Abdurakhmanov amesifu na kupongeza sana nafasi chanya ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusiana na kadhia ya Syria kama nchi moja wapo inayounga mkono usitishaji vita ndani ya taifa hilo la Kiarabu.

Magaidi wa Kiwahabi wanaochafua usalama nchini Syria

Kadhalika ripoti hiyo imeelezea sisitizo la, nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki juu ya azma yao ya kuendeleza juhudi kwa ajili ya mazungumzo ya Geneva. Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Kazakhstan, duru ya ijayo ya mazungumzo ya Astana, itafanyika tarehe tatu na tarehe nne za mwezi Mei na kikao kingine kitakachohudhuriwa na wataalamu wa masuala ya kiufundi, kitafanyika mwezi Aprili mjini Tehran.

Tags