Guterres aamuru kufutwa ripoti ya Apartheid kuhusu Israel
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameamuru kufutwa ripoti ya ESCWA kuhusu siasa za ubaguzi za utawala haramu wa Israel. Hatua hiyo ya Antonio Guterres imechukuliwa kutokana na mashinikizo ya waitifaki wa utawala huo ghasibu.
Duru za kidiplomasia zimetangaza kuwa Antonio Guterres Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameagiza kufutwa ripoti ya Kamati ya Kiuchumi na Kijamii ya Asia Magharibi katika Umoja wa Mataifa (ESCWA) kuhusu siasa za ubaguzi za Israel. Guterres ameachukua hatua hiyo kutokana na mashinikizo ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Kamati hiyo juzi Jumatano iliutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa umetenda jinai za kibaguzi yaani Apartheid dhidi ya raia wa Palestina. Baada ya kutolewa ripoti hiyo, serikali ya Marekani pia imemtaka Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aifute ripoti hiyo ya ESCWA kuhusu siasa za kibaguzi za Israel dhidi ya Wapalestina.
Antonio Guterres ameashiria katika ripoti yake aliyoitoa ndani ya Baraza la Usalama la Umoja huo kuhusu ulazima wa kupokonywa silaha harakati ya Hizbullah ya Lebanon na kuitaka harakati hiyo na makundi yote ya Lebanon kuacha kushiriki kivyovyote katika mapigano huko Syria.
Guterres pia ameyataja mashambulizi ya karibu kila siku ya ndege za kivita za Israel dhidi ya anga ya Lebanon kuwa ni ukiukaji wa wazi wa mamlaka ya kitaifa ya Lebanon na azimio nambari 1701 la Baraza la Usalama. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa aidha amesema kuwa hatua ya Israel ya kuendelea kukaliwa kwa mabavu eneo la kaskazini la kijiji cha al Ghajar na kando yake kuwa ni jambo linalotia wasiwasi.