PLO yaikosoa UN kwa kushinikiza kufutwa ripoti dhidi ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i26580-plo_yaikosoa_un_kwa_kushinikiza_kufutwa_ripoti_dhidi_ya_israel
Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Mataifa kuagiza kufutwa ripoti ya Kamati ya Kiuchumi na Kijamii ya Asia Magharibi katika Umoja wa Mataifa (ESCWA) kuhusu siasa za ubaguzi za Israel.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 19, 2017 03:58 UTC
  • PLO yaikosoa UN kwa kushinikiza kufutwa ripoti dhidi ya Israel

Harakati ya Ukombozi wa Palestina (PLO) imekosoa vikali hatua ya Umoja wa Mataifa kuagiza kufutwa ripoti ya Kamati ya Kiuchumi na Kijamii ya Asia Magharibi katika Umoja wa Mataifa (ESCWA) kuhusu siasa za ubaguzi za Israel.

Hanan Ashrawi, mwanachama wa Kamati Kuu ya PLO amesema kuwa, badala ya Umoja wa Mataifa kukubali mashinikizo ya kisiasa na vitisho kutoka taasisi za nje, ilipaswa kuwa wa kwanza kulaani jinai zilizofichuliwa na ripoti hiyo, sambamba na kuuwajibisha utawala haramu wa Israel kwa jinai zake.

Amemtaka Katibu Mkuu wa UN kutenda jambo la sawa kwa kuakisi hali halisi inayoshuhudiwa katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu, yakiwemo mauaji na ukandamizaji dhidi ya Wapalestina, pamoja na ukaliaji wa mabavu wa kijeshi.

Wakati huo huo, Riyad al-Maliki, Waziri wa Mambo ya Nje wa Palestina naye pia amelaani hatua hiyo ya UN akiielezea kuwa ni ya kujaribu kuficha uovu wa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa walimwengu.  

Rima Khalaf raia wa Jordan aliyejiuzulu kamati ya ESCWA

Jumatano iliyopita, Kamati ya Kiuchumi na Kijamii ya Asia Magharibi katika Umoja wa Mataifa (ESCWA) iliutuhumu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa umetenda jinai za kibaguzi yaani Apartheid dhidi ya raia wa Palestina. 

Duru za kidiplomasia zimetangaza kuwa, baada ya kutolewa ripoti hiyo, serikali ya Marekani pia ilimshinikiza Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteres aifute ripoti hiyo ya ESCWA kuhusu siasa za kibaguzi za utawala pandikizi wa Israel dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.

Rima Khalaf, Katibu Mtendaji wa ESCWA alitangaza kujiuzulu wadhifa wake baada ya Katibu Mkuu wa UN, kutoa amri ya kufutwa ripoti ya kamati hiyo inayoutambua utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa ni utawala wa kibaguzi, kuonesha upinzani na malalamiko yake dhidi ya hatua hiyo. 

Uzio wa kibaguzi wa utawala ghasibu wa Israel