Hamas: Israel ijiandae kwa jibu kali kwa kumuua kamanda wetu
(last modified Tue, 28 Mar 2017 16:27:56 GMT )
Mar 28, 2017 16:27 UTC
  • Hamas: Israel ijiandae kwa jibu kali kwa kumuua kamanda wetu

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imesema itatoa jibu kali kwa utawala wa Kizayuni wa Israel kwa kumuua mmoja wa makamanda wake waandamizi.

Khalid Mash'al, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas amesema kuwa: "Kwa kumuua Fuqaha, maadui zetu wametutumia ujumbe mzito kwamba wanaweza kuwaangamiza mashujaa wetu, tena katika kitovu cha Gaza. Uongozi wa kijeshi na kisiasa wa Hamas hauwezi kuufumbia macho ukatili huo, tuko tayari kupambana na wavamizi."

Ijumaa iliyopita, magaidi wenye mfungamano na utawala wa Kizayuni walimpiga risasi nne na kumuua shahidi Mazen Fuqaha, mateka wa Kipalestina aliyeachiliwa huru na ambaye alikuwa mmoja wa makamanda wa Brigedi za Izuddin al Qassam, tawi la kijeshi la Hamas katika eneo la Tel al Hawa, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Mazin Fuqaha, kamanda mwandamizi wa Hamas aliyeuliwa shahidi hivi karibuni

Mash'al ameongeza kuwa, kwa adui kuamua kuleta chokochoko zake katika maeneo ya Palestina ambayo yanaendeshwa na Hamas, Tel Aviv imeamua kubadili kikamilifu kanuni za msingi. Aidha amesisitiza kwamba nia na irada ya harakati ya muqawama ina nguvu kuliko zaidi silaha za maadui.

Fuqaha aliyekuwa na miaka 38, aliwahi kuzuiliwa katika jela ya utawala wa haramu wa Israel tangu mwaka 2003, na aliachiwa huru miaka 9 baadaye, katika fremu ya makubaliano  kubadilishana wafungwa ya Hamas na Tel Aviv. 

Tags