Magaidi 52 wa Daesh waangamizwa na jeshi la Iraq, Mosul
Jeshi la Iraq limewaangamiza wanachama 52 wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh/ISIS katika operesheni za kusafisha eneo la magharibi mwa mkoa wa Mosul.
Meja Ali Mohsen, Kamanda wa Kikosi cha Kupambana na Ugaidi cha Jeshi la Iraq (ICTF) amesema magaidi 17 wa Daesh wameuawa katika operesheni ya jana Jumatano katika eneo la al-Anbar, mbali na kuwatia nguvuni wanawake sita Waarabu wanachama wa genge hilo la kitakfiri.
Aidha kikosi hicho kimefanikiwa kukomboa asilimia 40 ya eneo la al-Arab katika operesheni ya pili ambapo makabiliano makali kati ya magaidi na wanajeshi wa Iraq yanaendelea kwa sasa.
Kamanda huyo kadhalika amesema magaidi wengine 20 wameuawa katika operesheni tofauti ya jeshi hilo katika eneo la al-Sabuniyah, huku wengine 15 wakiangamizwa katika eneo la Hadar, magharibi mwa mji wa Mosul.
Jumanne iliyopita, Msemaji wa Jeshi la Iraq, Brigedia Jenerali Yahya Rasool aliwaambia waandishi wa habari mjini Baghdad kuwa, Daesh ilikua inadhibiti asilimia 40 ya ardhi ya Iraq mwaka 2014, lakini kufikia Machi 31 mwaka huu, genge hilo la kigaidi lilikuwa linashikilia asilimia 6.8 tu ya ardhi ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi alisema kuwa ushindi dhidi ya kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh unakaribia huku akisisitizia umuhimu wa wananchi na jamii ya kimataifa kuendelea kuiunga mkono Iraq katika mapambano yake dhidi ya ugaidi.