Mkutano wa kusaka amani Syria unafanyika Tehran
(last modified Tue, 18 Apr 2017 03:52:37 GMT )
Apr 18, 2017 03:52 UTC
  • Mkutano wa kusaka amani Syria unafanyika Tehran

Mkutano wa wataalamu kuhusu mazungumzo ya amani Syria unafanyika leo mjini Tehran, Iran katika fremu ya mchakato wa amani wa Astana, Kazakhstan.

Kwa mujibu wa msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Bahram Qassemi, lengo la mkutano huo wa siku moja ni kuendeleza mazungumzo ya amani na njia za kufikia usitishaji vita Syria. Amesema mkutano huo mbali na wataalamu wa Iran pia utawashirikisha wataalamu kutoka Russia na Syria.

Qassemi amebainisha matumaini yake kuwa, mkutano huu ambao ni muendelezo wa vikao vilivyotangulia utakuwa na taathira nzuri katika kuendeleza mazungumzo ya kutafuta amani Syria.

Mazungumzo ya kusaka amani Syria yakifanyika Astana, Kazakhstan

Qassemi amesema kuwa, mkutano wa Astana 4 utafanyika Mei 4-5 mwaka huu katika mji huo mkuu wa Kazakhstan na kuongeza kuwa mkutano huo unaweza kuzaa matunda ya ushirikiano yanayotakiwa na Syria kwa kuzingatia jitihada za Iran, Russia na Uturuki.

Mazungumzo ya amani ya Syria hadi sasa yamefanyika mara kadhaa huko Astana kwa kuhudhuriwa pia na Iran, Russia na Uturuki kama nchi ambazo zilianzisha mazungumzo hayo ambayo yamekuwa yakiwashirikisha wawakilishi wa serikali ya Syria, makundi ya wabeba silaha na Staffan de Mistura, mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini Syria.