Ansarullah: Marekani na Israel ni pande mbili za sarafu moja
Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen, Abdul-Malik Badreddin al-Houthi amesema Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel ni pande mbili za sarafu moja ambazo kwa pamoja zinaunga mkono kwa hali na mali juhudi za kuibomoa na kuisambaratisha Yemen kupitia uvamizi wa kijeshi ulioanzishwa na Saudi Arabia.
Akihutubia Wayemen kupitia kanda ya video katika mji wa Sa'ada hapo jana, al-Houthi amesema dola la kibeberu la Marekani, utawala haramu wa Israel na waitifaki wao katika eneo la Mashariki ya Kati wanajaribu kushikiniza kufuatwa sera na 'thamani' zao katika nchi za kanda hii kwamba maadui hao wanaitazama Yemen kama chambo kisicho na maana cha kuweza kufanikisha maslahi yao katika eneo hili la kistratajia.
Kiongozi wa Harakati ya Ansarullah ya Yemen ameongeza kuwa: "Kwa mtazamo wa Marekani, vikosi huru vya majeshi ya Yemen, Syria, Lebanon na Iraq ni vikosi viovu vinavyotazamwa kwa jicho baya huku Washington inayojifanya kwamba ina huruma na mataifa hayo, ikitaka kuwageuza viongozi wa eneo hili kama vikaragosi."

Ametaja kuwa kichekesho na dhihaka madai yanayotolewa na Riyadh kuwa lengo lake la kuivamia Yemen ni kukomboa vijiji vya nchi hiyo maskini ya Kiarabu, jirani yake.
Itakumbukwa kuwa mwezi Machi mwaka 2015, kwa uungaji mkono wa Marekani, Saudi Arabia ilianzisha mashambulio dhidi ya maeneo mbalimbali ya Yemen. Moja kati ya malengo makuu ya mashambulio hayo ya kivamizi ya utawala wa Aal-Saud likiwa ni kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake, rais aliyejiuzulu na kuitoroka nchi Abdrabbuh Mansur Hadi.
Mbali na kuua na kujeruhi makumi ya maelfu ya raia, mashambulio ya Saudia yameteketeza pia miundombinu ya Yemen na kusababisha mamilioni ya Wayemen kubaki bila makazi na kuwa wakimbizi.