Mamilioni waadhimisha kumbukumbu ya kufa shahidi Imam Kadhim AS, Baghdad
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28184-mamilioni_waadhimisha_kumbukumbu_ya_kufa_shahidi_imam_kadhim_as_baghdad
Mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wamekusanyika katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Musa Kadhim AS, mmoja wa watu wa nyumba toharifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Apr 24, 2017 03:46 UTC
  • Mamilioni waadhimisha kumbukumbu ya kufa shahidi Imam Kadhim AS, Baghdad

Mamilioni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia wamekusanyika katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, katika maadhimisho ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Musa Kadhim AS, mmoja wa watu wa nyumba toharifu ya Bwana Mtume Muhammad SAW.

Licha ya vitisho vya mashambulizi ya kigaidi ya genge la kitakfiri la Daesh (ISIS), mamilioni ya waumini hao jana Jumapili ambapo ilikuwa kilele ya maadhimisho hayo, walifanya maandamano ya amani na kisha wakakusanyika katika Haram ya Imam Musa Kadhim AS, Imam wa 7 wa madhehebu ya Shia, katika wilaya ya Kadhimiyah, kaskazini mwa Baghdad.

Waandalizi wa maadhimisho haya wanakadiria kuwa watu zaidi ya milioni 6 wameshiriki katika kumbukumbu ya tukio hilo chungu mjini Baghdad, chini ya wingu la usalama na ulinzi mkali.

Genge la kigaidi la Daesh limekuwa likitekeleza mashambulizi ya kinyama ya mabomu nchini Iraq tangu mwezi Juni mwaka 2014.

Imam Musa Kadhim AS

Imam Mussa al-Kadhim AS alizaliwa mwezi 7 Mfunguo Tano Safar mwaka 128 Hijria katika eneo la al Abwaa nje kidogo ya mji mtakatifu wa Madina. 

Kiongozi huyo mwana wa kiume wa Imam Jaafar Swadiq AS, alishika hatamu za Uimamu na kuongoza umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35. Kipindi cha uimamu wake kilijaa misukosuko na mashaka mengi na kiliambatana na kuchanua utawala wa wafalme wa Bani Abbas.