Matukio ya hivi karibuni Mosul na udharura wa kuwa macho Wairaki
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i28452-matukio_ya_hivi_karibuni_mosul_na_udharura_wa_kuwa_macho_wairaki
Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, siku ya kukombolewa kikamilifu mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh (ISIS) imekaribia na wakati huo huo kutahadharisha juu ya changamoto za baada ya kukombolewa mji huo.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Apr 30, 2017 07:32 UTC
  • Matukio ya hivi karibuni Mosul na udharura wa kuwa macho Wairaki

Waziri Mkuu wa Iraq amesema kuwa, siku ya kukombolewa kikamilifu mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa Daesh (ISIS) imekaribia na wakati huo huo kutahadharisha juu ya changamoto za baada ya kukombolewa mji huo.

Haider al-Abadi, aliyasema hayo jana katika kongamano la 'Umoja wa Kitaifa' mjini Baghdad, mji mkuu wa nchi hiyo na kuongeza kuwa, baada ya kukombolewa mji wa Mosul, taifa la Iraq litaingia katika hatua mpya na kwamba, kulindwa umoja wa kitaifa, kuwarejesha wakimbizi katika makazi yao, kutoa huduma na kujenga upya miundombinu, ni changamoto muhimu zitakazolikabili taifa hilo baada ya ushindi dhidi ya magaidi. Haider al-Abadi ameongeza kuwa, pamoja na kwamba, jamii za wachache za Wakristo na Mayazidi zimekumbwa na mauaji ya kizazi yaliyofanywa na magaidi wa Daesh, lakini kwamba serikali haipasi kuruhusu kutokea ulipizaji kisasi mjini Mosul.

Jeshi la Iraq likiwa limeweka mzingiro dhidi ya magaidi

Ni kufuatia hali hiyo ndio maana Haider al-Abadi akasema kuwa, serikali yake inasisitizia maridhiano ya kitaifa kuchukua nafasi ya ulipizaji kisasi. Kadhalika amebainisha kwamba, njia pekee ya kukabiliana na fitina za kidini nchini Iraq ni sisitizo la umoja wa kitaifa na kujiepusha kuwabagua raia. Inaelezwa kwamba operesheni za kuukomboa mji wa Mosul haziwezi kulinganishwa na operesheni nyingine yoyote iliyowahi kujiri nchini Iraq. Hii ni kwa kuwa, mji huo una umuhimu mkubwa kwa pande zote za Iraq zinazoshughulishwa na mgogoro wa nchi hiyo. Aidha Mosul ni mji wenye umuhimu mkubwa kwa makundi ya kigaidi kwani ni makao makuu ya utawala wao na ngome ya mwisho kwa magenge hayo ya  kigaidi. Mbali na hayo ni kwamba Mosul ni mji wenye umuhimu wa kipekee kwa serikali ya Baghdad, kwani kwa kuwa na karibu watu milioni mbili, ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Iraq huku ukiwa na umuhimu pia wa kiuchumi. Ushindi wa serikali dhidi ya kundi la Daesh (ISIS) mjini Mosul, una maana ya kufikia tamati harakati za magaidi ndani ya taifa hilo sambamba na kulinda umoja wa ardhi yote ya Iraq.

Magaidi wakufurishaji wa Daesh (ISIS) wanaoungwa mkono na US na Saudia

Hali ikiwa ni hiyo, mji huo pia unaonekana kuwa na umuhimu mkubwa kwa Wakurdi wa Iraq, kwani baadhi ya maeneo ya Mosul yapo katika sehemu yenye kuzozaniwa baina ya serikali ya eneo la Kurdistan na serikali kuu ya Baghdad. Ni kwa kutilia maanani ukweli huo, ndio maana uendeshwaji wa mji huo baada ya kukombolewa kwake kutoka mikononi mwa magaidi, unaweza kubadilika na kuwa sababu kuu ya hitilafu kati ya Wakurdi na serikali ya Baghdad kutokana na uchochezi na njama za madola ya kibeberu ya Magharibi. Kadhalika mji wa Mosul una umuhimu wa aina yake kwa pande za kigeni hususan Marekani. Hii ni kwa kuwa uepo wa Waarabu wa Kisuni wanaounda asilimia kubwa ya wakazi wa mji huo, unatumiwa na Washington kwa ajili ya kupenyeza ushawishi na kutekeleza njama zake zenye lengo la kuibua fitina nchini Iraq.

Nembo ya Harakati ya Hashdu sh-Sha'abi inayoshirikiana na jeshi la Iraq kuwafurusha magaidi

Mabadiliko ya Iraq yanabainisha kwamba umoja wa Wairaki na kwa kutegemea nguvu yao ya asili, ndio sababu kuu ya mafanikio yao makubwa katika kukabiliana na genge la ukufurishaji la Daesh pamoja na mafanikio ya miezi ya hivi karibuni katika kukombolewa maeneo muhimu yaliyokuwa yakidhibitiwa na kundi hilo. Itafahamika kuwa karibu miaka mitatu iliyopita na kupitia njama za kimataifa na kieneo chini ya mipango kamili ya Marekani na baadhi ya madola tegemezi ya eneo la Mashariki ya Kati, kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) liliweza kudhibiti mji wa Mosul ambao ni moja ya miji muhimu sana nchini Iraq. Tangu mwezi Juni mwaka 2014, serikali ya Baghdad kwa kutegemea vikosi tofauti vya Iraq ikiwemo Harakati ya Kujitolea ya Wananchi ya Hashdu ash-Sha'abi, ilianzisha mapambano makali dhidi ya wanachama wa kundi hilo maarufu kwa kufanya jinai dhidi ya binaadamu. Ni vyema kufahamika kwamba, kundi hilo la kigaidi katika kukaribia mwisho wa uhai wake limekuwa likitenda jinai za kutisha kwa lengo la kutafuta upenyo wa kutoroka kutokana na kushindwa kwake kikamilifu nchini humo.

Mji wa Mosul, ambao ulikuwa umedhibitiwa na magaidi wakufurishaji

Kwa mantiki hiyo inatatajiwa kwamba jinai za kundi hilo yakiwemo matumizi ya silaha za kemikali zilizopigwa marufuku zitaongeza nchini humo katika siku zijazo. Uharibifu mkubwa wa miundombinu nchini Iraq hususan mjini Mosul, umekuwa mkubwa kiasi kwamba baadhi ya weledi wa mambo wanatabiri kwamba, ukarabati wake utachukua kwa akali miaka 10. Ala kulli hali, hadi sasa kundi la kigaidi la Daesh na waungaji mkono wake yaani Marekani, utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na nchi tegemezi za Kiarabu katika eneo la Mashariki ya Kati hususan Saudia, wamelisababishia hasara kubwa taifa la Iraq, na kwa ajili hiyo Wairaki wana matumaini kwamba hali hiyo itafikia kikomo kupitia operesheni za sasa za kuisafisha nchi yao. Ni suala lisilo na shaka kwamba, umoja baina ya makundi ya kisiasa, koo tofauti na raia wa Iraq, ndio siri ya ushindi na mafanikio ya taifa hilo katika kipindi hiki muhimu. Kufungamana nchi hiyo na demokrasia, kuimarisha mshikamano wa kisiasa, uwezo wake wa kiuchumi, kijeshi na juhudi za kuimarisha usalama na amani, kutalisaidia taifa hilo kufikia uwezo wake wa kimaendeleo na kujenga upya nchi. Na hiyo ndiyo nukta ambayo imesisitizwa na Haider al-Abadi,Waziri Mkuu wa Iraq katika matamshi yake ya hivi karibuni.