Al Zahar: Israel ni adui wa nchi zote za Kiislamu
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ni adui wa nchi zote za Kiislamu na kwamba njama za utawala huo pandikizi zinalenga kuuangamiza ulimwengu mzima wa Kiislamu.
Televisheni ya al Mayadeen ya nchini Lebanon imeripoti habari hiyo na kumnukuu Mahmoud al Zahar akizitaka nchi zote za Kiislamu kuuhesabu utawala wa Kizayuni wa Israel kuwa adui nambari moja wa umma mzima wa Kiislamu na hivyo ziunganishe pamoja nguvu zao na kuutia nguvu ulimwengu wa Kiislamu kupitia kuzuia kufanikishwa njama za utawala huo ghasibu.
Aidha ameilaumu Mamlaka ya Ndani ya Paletina kwa misimamo yake ya hivi karibuni dhidi ya Ukanda wa Ghaza na kudharau kwake matatizo ya mateka wa Palestina walioko katika jela za kutisha za Israel. Vile vile amemtuhumu Mahmoud Abbas, Rais wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kwa kusema kuwa, anatumia vibaya fedha na mali za Wapalestina.
Kiongozi huyo mwandamizi wa HAMAS pia amesisitizia udharura wa kulindwa umoja na mshikamano wa Wapalestina katika kupambana na njama za Wazayuni na kuwataka watu wenye fikra huru duniani kuunganisha nguvu zao katika kukabiliana na dhulma ya Israel ya kuuzingira kila upande Ukanda wa Ghaza.
Ikumbukwe kuwa, kwa miaka 10 sasa utawala wa Kizayuni wa Israel umeuzingira kila upande Ukanda wa Ghaza na unazuia kuingia hata mahitaji ya kimsingi kabisa ya wananchi wa ukanda huo kama vile madawa, vyakula na vifaa vya ujenzi.