Hizbullah yatoa radiamali na kukosoa Hati mpya ya Kisiasa ya Hamas
(last modified Wed, 03 May 2017 03:46:18 GMT )
May 03, 2017 03:46 UTC
  • Hizbullah yatoa radiamali na kukosoa Hati mpya ya Kisiasa ya Hamas

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon amesisitiza kuwa muqawama usiopigania kukomboa ardhi yote ya kihistoria ya Palestina hauwezi kuwa na tija wala faida yoyote.

Sheikh Naeem Qassim ameyasema hayo mjini Beirut, Lebanon alipokutana na ujumbe wa "Harakati ya Kimataifa ya Kurejea Palestina". Naibu Katibu Mkuu wa harakati ya muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ameashiria hati mpya ya kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ambayo imeridhia kuundwa ya Palestina katika mipaka ya ardhi zilizoanza kukaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel mwaka 1967 na kueleza kwamba muqawama ambao hautowarejesha Wapalestina kwa izza na heshima kwenye ardhi zao na usiopigania ukombozi wa ardhi yote ya kihistoria ya Palestina hauna faida yoyote.

Sheikh Naeem Qassim amesisitiza pia kwamba muqawama unaoigawa Palestina katika sehemu mbili haukubaliwi na Hizbullah na akaongezea kwa kusema, harakati inayoandaa mazingira ya kufanya mapatano ya wazayuni maghasibu haitetei muqawama.

Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah amebainisha kuwa maadamu wananchi wa Palestina wanaendelea kuvumilia machungu na mateso yanayotokana na uvamizi na jinai za Uzayuni na wako tayari kujitoa mhanga katika njia ya muqawama kuna matumaini makubwa ya kupatikana mafanikio.

Khalid Mash'al, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas

Hizbullah ya Lebanon imetoa radiamali hiyo baada ya Hamas, kupitia Mkuu wake wa Ofisi ya Kisiasa Khalid Mash'al kuzindua rasmi hati yake mpya ya kisiasa hapo jana; ambapo kwa mujibu wa vyombo vya habari katika hati hiyo kimefutwa kifungu kinachosisitiza "kuangamizwa utawala wa Kizayuni wa Israe". 

Hii ni katika hali ambayo Waziri Mkuu wa utawala huo ghasibu Benjamin Netanyahu ameibeza hatua hiyo ya Hamas na kueleza kuwa ni jaribio la kutaka kuuhadaa ulimwengu.../

Tags