Muqtada Sadr aitisha maandamano nje ya ubalozi wa Bahrain, Baghdad
Sayyid Muqtada Sadr, Kiongozi wa Harakati ya Sadr ya Iraq amewataka wananchi wa taifa hilo la Kiarabu wakusanyike nje ya ubalozi wa Bahrain mjini Baghdad, kulalamikia ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na viongozi wao nchini humo.
Amesema mwelekeo uliochukuliwa na serikali ya Manama wa kushadidisha jinai zake dhidi ya Mashia wa nchi hiyo yumkini ukalitumbukiza eneo zima la Mashariki ya Kati katika matatizo makubwa.
Kadhalika msomi huyo mtajika wa Iraq ametoa wito kwa wanawake nchini humo kujitokeza kushiriki maandamano kama ya leo nje ya ubalozi wa Bahrain mjini Baghdad hapo kesho.
Matamshi haya yanatolewa baada ya askari wa utawala wa Aal-Khalifa nchini Bahrain kuvamia eneo la Diraz na kuwashambulia Waislamu wanaomuunga mkono Sheikh Isa Qassim, kiongozi mkubwa wa Waislamu wa Shia, ambapo watu watano waliuawa shahidi huku makumi ya wengine wakijeruhiwa.
Katika hujuma hiyo askari wa utawala huo wa Aal-Khalifa walivamia makazi ya Ayatullah Isa Qassim na kuwatia mbaroni watu zaidi ya 280 waliokuwa ndani na nje ya nyumba hiyo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch zimelaani uvamizi huo, na kusema huwa ni ukandamizaji wa wazi wa uhuru wa kujieleza.