Jaafari: Iraq haitounga mkono muungano dhidi ya Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq amesema nchi yake katu haitounga mkono wala kushirikiana na muungano wowote uliopo au utakaoundwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Katika mahojiano na gazeti la ABC la Uhispania, Ibrahim al-Ja’afari amesema serikali ya Baghdad hata siku moja haiwezi kuunga mkono muungano dhidi ya Iran.
Ja'afari ameashiria kuhusu muungano ambao sio rasmi wa Marekani na baadhi ya nchi za Ghuba ya Uajemi hususan Saudi Arabia na kufafanua kuwa, Iraq haiwezi kufuata sera hizo za Washington zilizo dhidi ya Tehran.
Mwanadiplomasia huyo wa Iraq amesema Iran haijaghusubu hata inchi moja ya ardhi ya Iraq, katika hali ambayo nchi kama Uturuki imeingia umbali wa kilomita 110 ndani ya ardhi ya Iraq.
Matamshi ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iraq yanajiri siku chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kufanya ziara nchini Saudi Arabia, ambapo Washington ilisaini makubaliano ya mauzo ya silaha kwa Riyadh, yenye thamani ya dola bilioni 110 za Marekani.
Katika mkutano na viongozi wa nchi za Kiarabu mjini Riyadh, Trump alisisitiza kuhusu kuimarisha ushirikiano dhidi ya kile alichokitaja kuwa, nafasi hasi ya Iran katika eneo la Mashariki ya Kati.