UN: Daesh imeua raia 163 waliokuwa wakikimbia Mosul, Iraq
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i30130-un_daesh_imeua_raia_163_waliokuwa_wakikimbia_mosul_iraq
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeua raia 163 waliokuwa wakiukimbia mji wa Mosul nchini Iraq ndani ya wiki moja pekee.
(last modified 2026-01-14T08:12:18+00:00 )
Jun 06, 2017 23:18 UTC
  • UN: Daesh imeua raia 163 waliokuwa wakikimbia Mosul, Iraq

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh limeua raia 163 waliokuwa wakiukimbia mji wa Mosul nchini Iraq ndani ya wiki moja pekee.

Zeid Ra’ad al-Hussein aliyasema hayo jana Jumanne katika ufunguzi wa mkutano wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva, Uswisi na kuongeza kuwa, magaidi hao walifanya mauaji hayo ya umati ili kuwazuia raia hao kuuturoka mji huo, unaoshuhidia operesheni ya kijeshi ya kuzima harakati za kigaidi.

Amesema maafisa wa UN wamehesabu miili 163 ya raia wakiwemo wanawake na watoto wadogo katika barabara za eneo la al-Shira, magharibi mwa Mosul.

Wakati huo huo, Rupert Colville, Msemaji wa Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, yumkini mauaji hayo yalifanyika siku moja tu, yaani tarehe Mosi mwezi huu wa Juni.

Kaburi la umati lililoginduliwa hivi karibuni Mosul, likiwa na miili 60 ya raia

Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita, Dave Eubank, afisa wa shirika la kutoa misaada ya kibinadamu la Free Burma Rangers (FBR) aliliambia shirika la habari la Reuters kuwa, makumi ya miili ya raia waliouawa kinyama na Daesh imetapakaa katika barabara za eneo la Zanjili, magharibi mwa mji wa Mosul.

Zaidi ya raia laki saba wamefanikiwa kuukimbia mji wa Mosul lakini kuna watu wengine wapatao laki mbili ambao wameshindwa kukwepa mtego na mzingiro wa Daesh katika mji huo wa kistratajia, uliokuwa ukishikilia na mgaidi hao wakufurishaji.