Taathira za kieneo za mvutano wa Saudi Arabia na Qatar
(last modified Thu, 08 Jun 2017 15:28:43 GMT )
Jun 08, 2017 15:28 UTC
  • Taathira za kieneo za mvutano wa Saudi Arabia na Qatar

Mvutano katika uhusiano wa Saudi Arabia na Qatar bila shaka utakuwa na taathira kubwa hasi kwa utawala wa Riyadh katika upeo wa kieneo.

Hata kama kwa sasa Qatar ndiyo inayokabiliwa na mashinikizo makubwa ya ndani na nje ya nchi yanayotokana na kuharibika uhusiano huo lakini bila shaka ni Saudia ndiyo itakayobeba mzigo mzito zaidi wa taathira hasi za kuvurugika uhusiano huo katika muda mrefu. Taathira ya kwanza ni kuwa kuharibika uhusiano huo ambao umeathiri pia uhusiano wa Qatar na nchi nyingine za Kiarabu zikiwemo Imarati na Misri, tayari kumevuruga muundo wa kijeshi wa baadhi ya nchi za Kiarabu unaoongozwa na Saudia dhidi ya Yemen. Kwa ibara nyingine ni kwamba askari wa Qatar ambao wanaunda sehemu muhimu ya jeshi hilo la kivamizi tayari wameondolewa katika muungano huo na kurejeshwa nyumbani. Kujiondoa Qatar kwenye muungano huo kuna maana kwamba vyombo vya habari vya nchi hiyo na hasa televisheni ya habari ya Al-Jazeera, vitabadilisha msimamo wao kuakisi habari na kuanza kutangaza habari zinazokaribia ukweli wa mambo kuhusiana na jinai za kivita zinazotekelezwa na muungano huo wa Saudia huko Yemen na hivyo kuongeza mashinikizo ya fikra za waliowengi duniani dhidi ya siasa za jinai zinazotekelezwa na watawala wa Riyadh huko Yemen.

Uharibifu mkubwa unaofanywa na mashambulio ya Saudia katika maeneo ya makazi ya raia nchini Yemen

Taathira ya pili ni kwamba kuvurugika uhusiano wa Saudia na Qatar kuna maana ya kuvunjika umoja wa nchi za Kiarabu ambao ulijaribu kuonyeshwa na Saudia mwezi uliopita mjini Riyadh wakati wa kufanyika nchini humo safari ya Rais Donald Trump wa Marekani. Mvutano huo bila shaka utadhoofisha pia umoja na ushirikiano wa nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi na hivyo kuvuruga juhudi za kujaribu kubuni siasa moja zinazopaswa kufuatwa na nchi wanachama. Hii ni katika hali ambayo Saudia imekuwa ikilitegemea pakubwa baraza hilo kwa ajili ya kutekeleza siasa zake za kibabe katika eneo.

Trump alipokutana hivi karibuni na watawala wa Kiarabu mjini Riyadh

Taathira ya tatu ni kwamba mvutano kati ya Saudia na Qatar una maana ya kushindwa madai ya kubuniwa Nato ya Kiarabu katika eneo kwa uongozi wa watawala wa Riyadh. Katika miezi ya hivi karibuni watawala wa Aal Soud wamekuwa wakifanya jitihada kubwa za kuunda muungano wa kijeshi kwa lengo la kukabiliana na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lakini sasa kuharibika uhusiano wa nchi mbili hizo kumethibitisha wazi kwamba kufikiwa lengo hilo ni ndoto tu bali hata baadhi ya nchi muhimu za Kiarabu kama vile Qatar, Oman na Kuwait zinasisitiza udharura wa kuwa na uhusiano mzuri na Iran. Nukta ya nne ni kwamba kuharibika uhusiano wa Qatar na Saudia pia kunaweza kuathiri mgogoro wa Syria. Hata kama nchi mbili hizo yaani Saudia na Qatar zimekuwa zikifanya juhudi za kuingusha serikali halali ya Damascus lakini nchi hizo haziungi mkono makundi mamoja ya kigaidi. Mvutano wa hivi sasa wa nchi hizo unaweza kuipelekea Qatar kupunguza uungaji mkono wake kwa makundi ya kigaidi yanayojaribu kuiondoa madarakani serikali ya Damascus kwa njia zisizo za kisheria.

Amir wa Qatar akishiriki moja ya vikao vya wakuu wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi

Taathira ya tano inayotokana na kuvurugika kwa uhusiano wa Saudia na Qatar ni kwamba kuna uwezekano mkubwa wa kuvurugika uhusiano wa Saudia na Uturuki. Hata kama Uturuki imekuwa na uhusiano mzuri na Saudia katika miaka ya hivi karibuni lakini uhusiano wa Ankara na Doha ni mkubwa na imara zaidi kuliko wa nchi hiyo na Riyadh. Wakati huohuo uungaji mkono wa pamoja wa Uturuki na Qatar kwa Ikhwanul Muslimeen na vilevile kuundwa nchini humo kituo cha kijeshi cha Uturuki ni dalili ya wazi inayothibitisha uhusiano mkubwa uliopo kati ya nchi hizo. Kwa maelezo hayo ni wazi kuwa kuongezeka uungaji mkono wa Uturuki kwa Qatar katika mazingira ya hivi sasa kutakuwa na taathira hasi kwa nafasi ya kieneo ya Saudi Arabia.

Tags