HAMAS yasifu msimamo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar
(last modified Sun, 11 Jun 2017 08:03:03 GMT )
Jun 11, 2017 08:03 UTC
  • HAMAS yasifu msimamo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar

Msemaji wa Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS amesifu msimamo wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Muhammad bin Abdulrahman Al Thani wa kusisitiza kwamba Hamas ni harakati halali ya muqawama.

Fawzi Barhum, ameeleza kupitia taarifa kwamba matamshi hayo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar yanaonyesha thamani na misingi halisi ambayo Doha imeiweka kuhusiana na kadhia ya Palestina na muqawama wake halali na wa kisheria.

Siku chache nyuma Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar Muhammad bin Abdulrahman Al Thani alitangaza kuwa Hamas ni harakati ya muqawama na ina uhalali wa kisheria mbele ya nchi za Kiarabu.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar alibainisha kuwa nchi yake inaunga mkono taifa la Palestina na malengo yake matukufu ya kiadilifu pamoja na kufikiwa maridhiano ya kitaifa baina ya harakati za Hamas na Fat-h.

Muhammad bin Abdulrahman Al Thani

Itakumbukwa kuwa siku ya Jumanne iliyopita, Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia Adel al-Jubeir alitangaza kuwa ili kutatua mgogoro uliojitokeza baina ya nchi za Kiarabu, lazima Qatar iache kuiunga mkono Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS.

Jumatatu iliyopita, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain na Misri zilitangaza kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar. Nchi hizo, mbali na mambo mengine, zimeitaka serikali ya Doha ikomeshe uungaji mkono wake kwa harakati ya Hamas. Hata hivyo Qatar imesisitiza kuwa haitaruhusu mtu yeyote aingilie siasa za nje za nchi hiyo.../

Tags