Kundi la kwanza la wanajeshi wa Uturuki lawasili nchini Qatar
Serikali ya Qatar imetangaza kuwa kundi la kwanza la wanajeshi wa Uturuki limewasili katika mji mkuu wa nchi hiyo Doha katika utekelezaji wa makubaliano ya kijeshi yaliyofikiwa baina ya nchi mbili.
Baada ya kuwasili mjini Doha, askari hao wa Uturuki ambao ni wa kikosi cha nchi kavu cha jeshi la nchi hiyo walielekea kwenye kituo cha kijeshi cha Tariq bin Ziyad na kuanza mazoezi mbalimbali katika kambi hiyo.
Kikosi hicho cha wanajeshi wa Uturuki waliotumwa nchini Qatar kimeandamana na vifaru na silaha nzito nzito.
Bunge la Uturuki, hivi karibuni lilipitisha sheria ya kuruhusu kupelekwa askari wa nchi hiyo nchini Qatar.
Wanajeshi wa Uturuki wamewasili nchini Qatar katika hali ambayo kwa mashinikizo ya Marekani, mnamo tarehe 5 ya mwezi huu wa Juni, Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Bahrain na Misri zilitangaza uamuzi wa kuvunja uhusiano wao wa kidiplomasia na Qatar.
Mgogoro kati ya nchi hizo ulianza kwa kisingizio cha kutangaza Qatar kuyaunga mkono makundi ya muqawama katika eneo la Mashariki ya Kati ambayo yanaungwa mkono na Iran na kwamba kiujumla serikali ya Doha haifuati mkondo mmoja wa mataifa ya Kiarabu.../