Zarif: Russia kuanza kuondoa vikosi vyake Syria, ishara nzuri
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i3121-zarif_russia_kuanza_kuondoa_vikosi_vyake_syria_ishara_nzuri
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametaja hatua ya Russia kuanza kuondoa vikosi vyake Syria kuwa ni ishara nzuri.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Mar 15, 2016 11:27 UTC
  • Zarif: Russia kuanza kuondoa vikosi vyake Syria, ishara nzuri

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran ametaja hatua ya Russia kuanza kuondoa vikosi vyake Syria kuwa ni ishara nzuri.

Muhammad Javad Zarif ameyasema hayo akiwa safarini nchini Australia na kuongeza kuwa, hatua hiyo inaashiria kuwa serikali ya Moscow inaona kuwa hakuna udharura kwa vikosi hivyo kuendelea kusalia nchini humo wakati huu ambapo makubaliano ya usitishaji vita umerefushwa kwa wiki ya tatu. Kadhalika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepongeza hatua hiyo ya Russia kuanza kuondoa vikosi vyake nchini Syria. Ofisi ya Rais wa Syria imetangaza kuwa marais wa Russia na Syria wamekubaliana kupunguzwa idadi ya vituo vya anga vya jeshi la Russia nchini humo. Ofisi ya Rais wa Syria imeripoti kuwa katika mazungumzo ya simu aliyofanya jana Rais Vladimir Putin wa Russia na Rais wa nchi hiyo Bashar al-Assad, viongozi hao wawili wamekubaliana kuhusu kupunguzwa idadi ya vituo vya anga vya jeshi la Russia nchini Syria. Putin alisisitiza kuwa kuondoka kwa vikosi hivyo hakumaanishi kuhitimishwa operesheni za kijeshi za Russia katika ardhi ya Syria na kwamba vituo vya anga na vya majini vya Moscow vitaendelea na kazi zao nchini humo. Rais wa Russia ameongeza kuwa vikosi vya Russia vilivyoko nchini Syria vimewezesha kupatikana mazingira mwafaka kwa mchakato wa amani wa nchi hiyo. Itakumbukwa kuwa mnamo Septemba 30 mwaka uliopita wa 2015 na kwa ombi rasmi la serikali ya Syria, jeshi la Russia lilianzisha operesheni za mashambulio makali ya angani dhidi ya ngome za makundi ya kigaidi yaliyoko nchini Syria yanayoungwa mkono na nchi kadhaa za Kiarabu na za Magharibi ikiwemo Marekani. Wakati huohuo duru za habari zimeripoti kuwa tayari Russia imeanza kuondoa zana na vifaa vyake vya kijeshi nchini Syria.