Bunge la Iraq lasherehekea kukombolewa mji wa Mosul
Wabunge wa Iraq wamefanya sherehe kufurahia ushindi wa hivi karibuni na kukomblewa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa magaidi wa kitakfiri wa Daesh. Hatua hiyo imechukuliwa na Bunge la Iraq ili kuonyesha mshikamano wa Bunge na vikosi vya jeshi la nchi hiyo na harakati ya wananchi ya Hashdu Sha'abi.
Spika wa Bunge la Iraq, Salim al Jabouri ametoa shukrani zake na kuvipongeza vikosi vya majeshi ya Iraq na akasema, upo udharura wa kuungana na kuwa kitu kimoja wananchi wa Iraq baada ya kundi la Daesh kupata kipigo. Al Jabouri amesema kuwa, Iraq kuanzia sasa inapasa kutafakari kuhusu awamu inayofuata baada ya ushindi huo dhidi ya Daesh.
Wakati huo huo Hakim al Zamili, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Usalama na Ulinzi katika Bunge la Iraq amesema kuwa, baada ya kumalizika operesheni ya Mosul, itaanza oparesheni nyingine ya kuukomboa mji wa Talaafar. Amesema kukombolewa eneo hilo kunamanisha kudhaminiwa usalama kamili wa mji wa Mosul.
Vikosi vya Jeshi la Iraq Alhamisi iliyopita viliingia katika Msikiti wa al Nuri uliokuwa ukitumiwa na kiongozi wa kundi la Daesh magharibi mwa Mosul na kama alivyosema Haidar al Abadi Waziri Mkuu wa Iraq, mafanikio hayo ni sawa na kufikia utawala wa Daesh huko Mosul.