Waziri Mkuu wa Iraq atangaza rasmi ushindi dhidi ya ISIS Mosul
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i31550-waziri_mkuu_wa_iraq_atangaza_rasmi_ushindi_dhidi_ya_isis_mosul
Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi ametangaza rasmi ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh katika mji wa Mosul miezi minane baada ya kuanza vita dhidi ya magaidi hao wakufurishaji.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 09, 2017 09:46 UTC
  • Waziri Mkuu wa Iraq atangaza rasmi ushindi dhidi ya ISIS Mosul

Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi ametangaza rasmi ushindi dhidi ya kundi la kigaidi la ISIS au Daesh katika mji wa Mosul miezi minane baada ya kuanza vita dhidi ya magaidi hao wakufurishaji.

Katika taarifa, Ofisi ya al-Ibadi imesema, "Amiri Jeshi Mkuu, Waziri Mkuu Haider al-Abadi, amewasili katika mji uliokombolewa wa Mosul na kuwapongeza wapiganaji shujaa na watu wa Iraq kwa ushindi wao mkubwa."

Tangazo hilo limekuja baada ya televisheni ya taifa kutangaza kuwa wanajeshi wamefika katika ukingo wa Mto Tigris na kupeperusha bendera ya Iraq eneo hilo. Hilo lilikuwa eneo la mwisho ambalo magaidi wa ISIS walikuwa wamekimbilia mjini Mosul. Idadi kubwa ya magaidi hao walijirusha ndani ya mto  na kujiangamiza mapema Jumapili baada ya kushindwa.

Wanajeshi wa Iraq wakisherehekea ushindi

Furaha na shangwe imeenea kote katika mji wa Mosul na Iraq kwa ujumla baada ya kuangamizwa kijeshi magaidi wa ISIS ambao walikuwa wameutangaza mji huo kuwa mji mkuu wa khilafa yao bandia tokea mwaka 2014.

Magaidi wa ISIS wametekeleza uharibifu mkubwa mjini Mosul na kuwaua maelfu ya raia  huku wengine takribani milioni moja wakikimbia makazi yao. Inakadiriwa kuwa ukarabati wa mji huo utagharimu takribani dola bilioni moja. Kutimuliwa ISIS mji wa Mosul na kukaribia kutimuliwa magaidi hao katika mji wanaoukalia wa Raqqa nchini Syria kunaashiria kuangamizwa kundi hilo la magaidi wa Kiwahhabi ambao wamekuwa wakitekeleza jinai na ukatili usio na kifani katika nchi hizo. Hivi sasa wakuu wa Iraq wanasema baada ya kushindwa kijeshi ISIS, kazi kubwa itakuwa ni kutokomeza fikra na idiolojia potovu ya utakfiri inayoenezwa na magaidi hao.