Jul 14, 2017 08:03 UTC
  • Maafisa wa Saudia waliwasaidia magaidi wa ISIS huko Mosul, Iraq

Saudi Arabia ilituma maafisa wake wa kijasusi na kijeshi kujiunga na magaidi wa ISIS au Daesh Mosul wakati wa oparesheni ya jeshi la Iraq ya kuukomboa mji huo.

Kwa mujibu wa  gazeti la al Sharq la Qatar, maafisa 150 wa kijeshi na kijasusi wa Saudi Arabia walijiunga na magaidi wa Kiwahabbi wa ISIS kwa lengo la kurefusha mapigano ya kuukomboa mji huo wa pili kwa ukubwa Iraq.

Gazeti hilo limefichua kuwa, wanajeshi wa Iraq wamepata nyaraka muhimu zinazothibitisha wazi kuwa maafisa wa kijasusi wa Saudia walikuwa wakitoa msaada kwa magaidi wa ISIS.

Siku ya Jumatatu Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi alitangaza rasmi kukombolewa mji wa Mosul ambao ulikuwa ngome ya magaidi wa ISIS toka Juni mwaka 2014. Mji huo umekombolewa na jeshi la Iraq kwa ushirikiano na jeshi la kujitolea la wananchi maarufu kama Hashdu Ash-Shaabi.

Wanajeshi wa Iraq wakilinda doria Mosul baada ya ISIS kutimuliwa

Magaidi wa ISIS wametekeleza uharibifu mkubwa mjini Mosul na kuwaua maelfu ya raia  huku wengine takribani milioni moja wakikimbia makazi yao. Inakadiriwa kuwa ukarabati wa mji huo utagharimu takribani dola bilioni moja.

Kutimuliwa ISIS mji wa Mosul na kukaribia kutimuliwa magaidi hao katika mji wanaoukalia wa Raqqa nchini Syria kunaashiria kuangamizwa kundi hilo la magaidi wa Kiwahhabi ambao wamekuwa wakitekeleza jinai na ukatili usio na kifani katika nchi hizo.

Hivi sasa wakuu wa Iraq wanasema baada ya kushindwa kijeshi ISIS, kazi kubwa itakuwa ni kutokomeza fikra na idiolojia potovu ya utakfiri inayoenezwa na magaidi hao.

 

Tags