Haider al-Abadi: Hashdu sh-Sha'abi Iraq haitovunjwa, itaendelea kuwepo
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i32750-haider_al_abadi_hashdu_sh_sha'abi_iraq_haitovunjwa_itaendelea_kuwepo
Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi amesema kuwa, harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi kamwe haitovunjwa na itaendelea kuwepo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 05, 2017 22:39 UTC
  • Haider al-Abadi: Hashdu sh-Sha'abi Iraq haitovunjwa, itaendelea kuwepo

Waziri Mkuu wa Iraq, Haider al-Abadi amesema kuwa, harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi kamwe haitovunjwa na itaendelea kuwepo.

Al-Abadi ameyasema hayo leo katika kongamano lililopewa jina la 'Fatwa ya Jihadi na Ushindi' ambalo limefanyika mjini Baghdad, mji mkuu wa Iraq na kuongeza kuwa, harakati hiyo ya wananchi wa Iraq iko chini ya serikali ya nchi hiyo na viongozi wa kidini wa mji wa Najaf na kwa msingi huo kamwe haitovunjwa.

Askari wa Iraq wakifurahia ushindi

Akiashiria kukaribia muda wa kukombolewa maeneo mengine ambayo bado yanadhibitiwa na kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS), Waziri Mkuu wa Iraq amevitaka vikosi vyote vya jeshi la nchi hiyo kushiriki katika operesheni ya kuyakomboa maeneo hayo na kwamba hadi sasa maandalizi ya kukomboa mji wa Tal Afar yanaendelea.

Tarehe 26 Novemba mwaka jana Bunge la Iraq lilipitisha kwa wingi wa kura muswada wa kuitambua rasmi harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi nchini humo. Harakati hiyo iliundwa na makundi tofauti ya Wairaq kufuatia wito wa Ayatullah Sistani, Marjaa na kiongozi mkubwa wa Waislamu wa Shia nchini humo baada ya kundi la kigaidi la Daesh kuudhibiti mji wa Mosul na kuutangaza kuwa makao makuu ya kile lilichokiita kuwa ni Dola la Khilafa hapo tarehe 10 Juni 2014. 

Mmoja wa makamanda wa harakati hiyo ya wananchi

Tangu wakati huo hadi leo jeshi la Iraq kwa kushirikiana bega kwa bega na harakati hiyo ya wananchi, limeweza kukomboa maeneo mengi ya nchi hiyo ukiwemo mji wa Mosul na kusambaratisha harakati za kundi hilo ndani ya ardhi ya nchi hiyo.