Mahmoud al-Zahar: Hamas iko tayari kushirikiana na wanaotaka kukombolewa Palestina
Mjumbe mwandamizi wa ofisi ya kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesema kuwa, harakati hiyo iko tayari kushirikiana na watu wote wanaofanya juhudi za kutaka kukombolewa Palestina kutoka katika makucha ya Wazayuni maghasibu.
Dakta Mahmoud al-Zahar ambaye ni kiongozi wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS amesisitiza kwamba, harakati hiyo inajitenga kuwa na uhusiano wa aina yoyote ile na watu ambao wanaifanyia uhaini na usaliti kadhia ya Palestina na inalaani vikali usaliti huo.
Dakta Zahar sambamba na kubainisha adhama ya muqawama wa Palestina katika nguvu na uwezo licha ya kuweko mzingiro wa kila upande ameeleza kuwa, kila mtu ambaye anatafuta njia sahihi basi anapaswa kubeba silaha na kukabiliana na utawala ghasibu wa Israel ambao unatenda jinai kila uchao dhidi ya wananchi madhulumu wa Palestina.
Wiki iliyopita Kanali ya Pili ya Televisheni ya utawala haramu wa Israel ilitangaza kuwa, hadi sasa Ukanda wa Gaza haujasalimu amri mbele ya mashinikizo ya utawala huo na katu hautasalimu amri na kwamba, katika mipango ya muqawama wa Palestina hakuna kitu kinachojulikana kwa jina la kuweka chini silaha ili hali ya uchumi iboreshwe.
Hivi sasa ni zaidi ya miaka kumi tangu utawala wa Kizayuni wa Israel uanze kutekeleza mzingiro dhidi ya eneo la Ukanda wa Gaza, ambapo umekuwa ukizuia pia kufikishiwa huduma muhimu wananchi hao madhlumu.