Hamas yasisitiza nia njema ya Iran kuhusu kadhia ya Palestina
Afisa wa Uhusiano wa Nje wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) amesema kuwa, nia njema ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kushughulikia suala la Palestina imethibitika wazi.
Usama Hamdani amesisitiza kuwa, uhusiano kati ya harakati ya Hamas na Iran una historia ya miaka 25 na ungali unaendelea. Hamdan ameongeza kuwa, Hamas ipo tayari kuanzisha uhusiano na nchi zote katika fremu ya maslahi ya Wapalestina na kwamba, misimamo ya nchi hizo kuhusu suala la Palestina na uungaji wao mkono kwa wananchi wa Palestina, haki na mapambano ya ukombozi vinapasa kuwa msingi wa uhusiano huo.
Afisa huyo wa Uhusiano wa Nje wa Hamas ameendelea kubainisha kuwa, mapambano ya kuzikomboa ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu ma Isarel yanaendelea na kwamba mapambano hayo hayatamalizika hadi ardhi zote za Palestina zitakapokombolewa.
Usama Hamdani pia amepinga vikali madai ya gazeti la al Riyadh la nchini Saudia lililoitaja harakati ya Hamas ya Palestina kuwa ni kundi la kigaidi na kisha gazeti hilo likalazimika kuifuta habari hiyo katika ukurasa wake wake wa intaneti baada ya kukabiliwa na mashinikizo na ukosoaji mkubwa. Amesema kwamba: Malalamiko ya wananchi ndani ya nje ya Saudi Arabia dhidi ya hatua hiyo ya gazeti la al Riyadh ni ujumbe wa wazi wa namna Palestina inavyopewa umuhimu na raia wa nchi za eneo hili.