WHO yatoa indhari baada ya Wayemeni nusu milioni kukumbwa na kipindupindu
Shirika la Afya Duniani WHO limetangaza kuwa kutokana na kuendelea hujuma na mashambulio ya kijeshi ya Saudi Arabia nchini Yemen, zaidi ya watu laki tano na elfu tatu wamekumbwa na ugonjwa wa kipindupindu nchini humo huku wagonjwa 1,975 wakiwa tayari wameaga dunia kuanzia mwezi Aprili mwaka huu hadi sasa kutokana na ugonjwa huo.
Katika ripoti liliyotoa jana Jumatatu, WHO limetangaza kuwa japokuwa kasi ya kuenea kipindupindu nchini Yemen imepungua katika kipindi cha kuanzia mwezi uliopita wa Julai hadi sasa lakini kila siku watu wapatao elfu tano wanaendelea kuambukizwa ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani limeeleza kuwa hali hiyo imesababishwa na mazingira na hali mbaya ya huduma za afya na tiba na mamilioni ya Wayemeni kukosa maji safi na salama ya kunywa.
Wakati huohuo Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom amesema maelfu ya watu ni wagonjwa nchini Yemen lakini hakuna kiwango cha kutosha cha hospitali, dawa na maji safi kwa ajili ya watu hao.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa WHO zaidi ya watu milioni 15 wanashindwa kupata hata suhula chache za tiba nchini humo.
Mashambulio ya anga yanayofanywa mtawalia usiku na mchana na ndege za kivita za Saudi Arabia nchini Yemen yameshaua watu zaidi ya 12,000 hadi sasa, wakiwemo wanawake na watoto na kuwafanya wengine zaidi ya milioni tatu wabaki bila ya makaazi tangu utawala huo wa Aal Saud ulipoanzisha vita dhidi ya nchi hiyo mwezi Machi mwaka 2015 kwa madhumuni ya kuisambaratisha harakati ya wananchi ya Ansarullah na kumrejesha madarakani kibaraka wake aliyekuwa rais wa nchi hiyo Abd Rabbuh Mansur Hadi.../