Mamia ya mahujaji wanusurika na ajali ya moto Makkah, Saudia
Mamia ya mahujaji wamenusurika katika ajali ya moto uliotokea katika jengo la ghorofa 15 mjini Makkah, Saudi Arabia.
Naif Al Sharif, msemaji rasmi wa polisi wa uokoaji nchini Saudia amesema kuwa, katika harakati za kuzima moto huo, jeshi hilo limefanikiwa kuwaokoa mahujaji 600 waliokuwa wamekwama katika jengo hilo ambao wanatoka mataifa ya Yemen na Uturuki na kwamba hakuna mtu aliyefariki dunia katika ajali hiyo.

Kadhalika polisi ya Saudia imesema kuwa, inaendelea na uchunguzi kubaini chanzo cha moto huo ambao ulianzia katika gorofa ya nane katika mfumo wa kuingiza baridi ndani ya jengo hilo.
Kabla ya hapo pia na katika kuthibitisha udhaifu wa utawala wa Aal-Saud kuhusiana na kushindwa kwao kusimamia usalama na utukufu wa mahujaji, jengo jingine la mahujaji wa Nyumba ya Mwenyezi Mungu (al-Kaaba) mjini Makkah iliwaka moto. Inafaa kuashiria kuwa, usimamizi mbovu wa viongozi wa Saudia katika kusimamia ibada ya Hijja husababisha vifo vya mamia ya mahujaji kila mwaka, huku tukio baya kabisa likiwa ni lile la maafa ya Mina lililotokea miaka miwili iliyopita kwa kusababisha vifo vya zaidi ya Mahujaji 7000.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na viongozi wa Saudia, idadi ya mahujaji wa kigeni ilipungua mwaka jana na kufikia karibu asilimia 20 kiasi kwamba ni mahujaji pekee milioni moja na laki nane ndio walioshiriki ibada hiyo mwaka huo. Hii ni katika hali ambayo katika miaka ya nyuma idadi hiyo ilikuwa inavuka watu milioni tatu.