Sisitizo la Qatar la kuimarisha uhusiano na Iran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar imesema usiku wa kuamkia leo Alkhamisi kwamba Doha imeamua kumrejesha balozi wake mjini Tehran.
Wizara hiyo imesema katika ripoti yake maalumu kwamba, uamuzi wa Qatar wa kumrejesha balozi wake nchini Iran unalenga kuimarisha zaidi uhusiano baina ya nchi hizi mbili ndugu na jirani. Qatar ilimwita nyumbani wake balozi wake aliyekuwepo hapa Tehran kutokana na mashinikizo ya Saudi Arabia.
Hivi majuzi pia, Waziri wa Ulinzi wa Qatar alisisitiza kuwa, ni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndiyo iliyoipa uhai mpya Qatar kwa kufungua mipaka yake ya anga kwa ajili ya ndege za Qatar, baada ya Saudia na wenzake kuiwekea vikwazo vya kidhulma Doha. Khalid bin Mohammad Al Attiyah aliongeza kuwa, hatua ya Iran ya kufungua mipaka yake ya anga kwa ajili ya ndege za Qatar, ilidhamini baadhi ya mahitaji muhimu ya Qatar katika wakati mgumu sana, hasa chakula.
Tarehe 5 Juni 2017, Saudi Arabia iliongoza kundi la nchi nne za Kiarabu, Misri, Imarati na Bahrain pamoja na Saudia yenyewe, kuiwekea vikwazo vya kila namna Qatar ikiwa ni pamoja na kukata uhusiano waoe wote na kuifungia mipaka yake yote ya ardhini, angani na baharini. Nchi hizo nne za Kiarabu zinadai kuwa, Qatar haikubali kufuata siasa za mrengo huo wa Kiarabu unaoongozwa na Saudi Arabia.
Tarehe 23 mwezi huo huo wa Juni, nchi hizo nne zilitoa orodha ya mambo 13 kama masharti ya kurejesha uhusiano wa kawaida na Qatar. Miongoni mwa masharti muhimu zaidi kati ya hayo 13 ni kuitaka Qatar ikate uhusiano wake na Iran pamoja na Hizbullah ya Lebanon na pia makundi ya mpambano ya Kiislamu ya Palestina kama vile HAMAS.
Hata hivyo Doha ilisimama kidete kupinga masharti yote hayo ya Saudia na kundi lake na ilisema kuwa, masharti hayo hayaingii akilini, bali yanalenga moja kwa moja kuipokonya Qatar uhuru wake wa kujitawala na kujiamulia yenyewe mambo yake. Kimsingi ni kwamba, baada ya Marekani kupata yakini kwamba haiwezi kufanikiwa katika siasa zake za kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itengwe kieneo na kimataifa, iliamua kuzitumia nchi za Kiarabu hasa Saudi Arabia kufanikisha malengo yake hayo ya kibeberu. Saudia iliyokubali kutekeleza siasa hizo za Marekani, ilijigamba kuwa imeundwa NATO ya nchi za Kiarabu ili kukabiliana na Iran, hata hiyo muungano huo ulisambaratika hata kabla ya kuanzishwa kwake. Qatar ni moja ya nchi za Kiarabu ambazo hazikubali kuburuzwa na Saudi Arabia jambo ambalo linawakasirisha mno viongozi wa Riyadh na kuamua kuchukua hatua kali za kuiadhibu Doha. Qatar ilisema kuwa, Saudi Arabia inaunda muungano wa namna hiyo ili kujinufaisha binafsi na kujifanya bora mbele ya nchi nyingine za Kiarabu. Upinzani huo wa Doha ulikuwa na maana ya kushindwa njama za Riyadh na kuanzisha muungano wa NATO wa nchi za Kiarabu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Kimsingi si Qatar pekee inayopinga siasa hizo za Saudi Arabia, bali nchi nyingine za Kiarabu kama Oman na Kuwait nazo zinasisitizia haja ya kuwa na uhusiano mzuri na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Maana ya maneno hayo ni kwamba, tofauti na ilivyotarajia Saudia Arabia, njama zake dhidi ya Iran zimeshindwa, bali kimsingi ni Riyadh ndiyo iliyotengwa na baadhi ya marafiki zake wa jana, kutokana na siasa zake hizo mbovu. Ukweli wa mambo ni kuwa Iran ni nchi kubwa yenye ushawishi kieneo na kimataifana yenye udiplomasia imara, hivyo kufikiria kuipuuza na kudhani nchi fulani inawezai kuifanya nchi kubwa kama hiyo itengwe kieneo na kimataifa, ni ndoto za alinacha.