Iraq yaishukuru Iran kwa misaada yake muhimu kwa serikali ya Baghdad
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33730-iraq_yaishukuru_iran_kwa_misaada_yake_muhimu_kwa_serikali_ya_baghdad
Balozi wa Iraq nchini Algeria ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwa nchi ya kwanza kuwasaidia wananchi wa Iraq katika wakati mgumu hasa wakati wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh walipokaribia kuutwaa mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 28, 2017 10:19 UTC
  • Iraq yaishukuru Iran kwa misaada yake muhimu kwa serikali ya Baghdad

Balozi wa Iraq nchini Algeria ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kuwa nchi ya kwanza kuwasaidia wananchi wa Iraq katika wakati mgumu hasa wakati wanachama wa kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh walipokaribia kuutwaa mji mkuu wa nchi hiyo, Baghdad.

Abdulrahman Hamid Mohammed Al-Hussaini, balozi wa Iraq nchini Algeria ameyasema hayo Jumatatu ya leo katika mazungumzo na Shirika la Habari la IRNA na kuongeza kuwa, Iran ina mchango mkubwa katika ushindi wa hivi karibuni wa wananchi wa Iraq dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh. Amesisitiza kuwa serikali na raia wa Iraq wana deni kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutokana na ushindi huo mkubwa. Abdulrahman Hamid Al-Hussaini amezungumzia mahusiano chanya kati ya Iran na Iraq na kusema kuwa, hivi sasa mataifa hayo yana mahusiano mazuri sana katika nyanja zote zikiwemo za uchumi na biashara.

Wanachama wa Daesh wakifanya jinai dhidi ya Wairaq

Balozi wa Iraq nchini Algeria amesema kuwa, hivi sasa kundi la Daesh limepata pigo kubwa katika uwanja wa vita na hata kifikra na kwamba karibu sana tu hivi, historia ya kundi hilo itatupwa katika madebe ya taka nchini Iraq. Kundi la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) chini ya uungaji mkono wa Marekani, Saudia na baadhi ya nchi za Magharibi na Kiarabu lilidhibiti miji mingi ya Iraq mwaka 2014 hususan maeneo ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo. Tangu wakati huo jeshi la Iraq kwa kushirikiana na harakati ya wananchi ya Hashdu sh-Sha'abi na misaada ya ushauri wa kijeshi ya Iran, limekuwa likipata ushindi na kusonga mbele  katika maeneo yaliyokuwa yanadhibitiwa na mgaidi wa Daesh na hivi sasa magaidi hao wamefurushwa katika maeneo yote muhimu ya Iraq.