Iran: Nchi yoyote haina haki ya kuiamulia Syria mambo yake
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, wananchi wa nchi za eneo hili ndio waamuzi wakuu wa mambo ya nchi zao na kwamba nchi yoyote haina haki ya kuwapangia cha kufanya wananchi wa Syria.
Hossein Jaberi Ansari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran katika masuala ya Kiarabu na Kiafrika alisema hayo jana (Jumatatu) hapa mjini Tehran mbele ya waandishi wa habari baada ya mazungumzo yake na Staffan De Mistura, mjumbe maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa katika suala la Syria na kuongeza kuwa, mazungumzo yake na De Mistura yamejadili juhudi za kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria kupitia mazungumzo ya amani ya Astana yanayosimamiwa na Iran, Russia na Uturuki. Aidha amesema, duru ya sita ya mazungumzo hayo itafanyika katikati ya mwezi ujao wa Septemba huko Astana, mji mkuu wa Kazakhstan.
Amesema, mazungumzo yanaendelea baina ya nchi tatu za Iran, Russia na Uturuki kuhusiana na tarehe hasa ya kikao hicho cha kimataifa cha Astana.
Amma kuhusiana na madai ya mirengo ya Kizayuni ya kuwa Iran inajaribu kueneza ushawishi wake katika eneo hili na hasa nchini Syria, Jaberi Ansari amesema, tangu mwanzoni kabisa mwa mgogoro wa Syria na migogoro mingine ya eneo hili, Tehran imekuwa na msimamo thabiti wa kufanya juhudi zake zote kutatua migogoro hiyo kwani inaamini kuwa kuenea migogoro katika eneo hili ni kwa madhara ya mataifa yote ya Mashariki ya Kati.
Kwa upande wake, Staffan De Mistura amewaambia waandishi wa habari kuwa kuna mabadiliko makubwa ya kisiasa na kijeshi na katika suala zima la kupambana na genge la kigaidi la Daesh (ISIS) nchini Syria.