WFP yaikosoa Saudia kwa kusababisha mgogoro wa kibinadamu Yemen
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i33951-wfp_yaikosoa_saudia_kwa_kusababisha_mgogoro_wa_kibinadamu_yemen
Mpango wa Chakula Duniani wa Umoja wa Mataifa WFP umeukosoa moja kwa moja utawala wa kifalme wa Aal-Saud kwa kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu nchini Yemen.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 05, 2017 09:38 UTC
  • WFP yaikosoa Saudia kwa kusababisha mgogoro wa kibinadamu Yemen

Mpango wa Chakula Duniani wa Umoja wa Mataifa WFP umeukosoa moja kwa moja utawala wa kifalme wa Aal-Saud kwa kusababisha mgogoro mkubwa wa kibinadamu nchini Yemen.

David Beasley, Mkurugenzi Mkuu wa WFP amesema Saudi Arabia inabeba dhima ya mgogoro huo na kwamba inafaa kukomesha mara moja mauaji ya watu wasio na hatia katika nchi hiyo jirani yake.

Amesema Saudia ina machaguo matatu, ima isitishe vita dhidi ya Yemen, itoe asilimia 100 ya misaada ya kibinadamu inayohitajika kwa wanachi wa taifa hilo au yote mawili.

Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amebainisha kuwa: "Saudia imesababisha mgogoro mkubwa wa kibindamu nchini Yemen; na hatua yake ya kuweka mzingiro katika bandari ya Hudaidah na kuharibu winchi za bandari hiyo kumevuruga kabisa juhudi za kufikisha misaada ya kibinadamu kwa wananchi wa Yemen."

Sehemu ya athari za hujuma za anga za Saudia nchini Yemen

Utawala wa Aal-Saud ulianzisha mashambulio ya kijeshi dhidi ya Yemen tangu mwezi Machi 2015 kwa uungaji mkono wa Marekani na baadhi ya nchi za Kiarabu za eneo hili. Mashambulio hayo hadi sasa yameshaua zaidi ya Wayemeni 12,000 na kuwajeruhi maelfu ya wengine, wengi wao wakiwa ni wanawake na watoto wadogo. 

Mkurugenzi Mkuu wa WFP ameongeza kuwa, vikwazo vilivyowekwa na muungano wa kijeshi wa Saudia nchini Yemen vimesababisha kuwa na ugumu katika kupeleka mafuta yanayotumiwa na magari ya Umoja wa Mataifa yanayoingia na kutoka katika nchi hiyo maskini ya Kiarabu.